KONGANI YA VIWANDA VYA DAWA KUPANUA AJIRA NA UWEKEZAJI

May 09, 2026
Serikali imeendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa dawa na vifaa tiba barani Afrika kupitia uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya afya na matumizi ya teknolojia za kisasa.

Kauli hiyo imetolewa leo Mei 8, 2026 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la uendelezaji wa kongani ya viwanda vya dawa na vifaa tiba.

Waziri Mchengerwa amesema hatua hiyo inalenga kupunguza utegemezi wa bidhaa za afya kutoka nje ya nchi sambamba na kuongeza uwezo wa ndani wa uzalishaji wa dawa, chanjo na vifaa tiba vinavyokidhi mahitaji ya wananchi na soko la kimataifa.

Amesema maendeleo ya kongani hiyo yatafungua fursa kubwa za ajira kwa vijana, kuongeza ushindani wa viwanda vya ndani na kuimarisha usalama wa afya nchini.

“Serikali imeamua kuwekeza katika sekta ya afya si kwa ajili ya utoaji wa huduma pekee, bali pia kama nguzo muhimu ya maendeleo ya uchumi wa taifa,” amesema Waziri Mchengerwa.

Aidha, amesema mfumo wa kongani utasaidia kupunguza gharama za uwekezaji kwa kuweka pamoja miundombinu muhimu ikiwemo maabara, mifumo ya maji, umeme pamoja na huduma za udhibiti wa ubora wa bidhaa za afya.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, hatua hiyo itawavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza kwa urahisi zaidi katika sekta ya dawa na vifaa tiba.

Pia amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na taasisi za elimu ya juu katika kujenga wataalamu wenye uwezo wa kuendesha viwanda vya kisasa vya dawa na teknolojia za afya nchini.

Ameongeza kuwa Tanzania inaendelea kujenga mazingira bora ya uwekezaji yatakayowezesha bidhaa za afya zinazozalishwa nchini kukidhi viwango vya kimataifa na kushindana katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, Dkt. Johanes Lukumay amesema Serikali imeendelea kuipa sekta ya Afya  msukumo wa juu ili kufikia hatua ya kujitegemea katika uzalishaji wa dawa hatua inayoweka msingi imara wa mageuzi makubwa ya kimkakati kuwekeza kwenye sekta hiyo. 

“Dira ya maendeleo ya Taifa ya miaka mitano inalenga kuhakikisha Tanzania inajenga uwezo wa kujitegemea katika uzalishaji wa dawa na vifaa tiba ifikapo mwaka 2030, sambamba na kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi,” amesema Dkt. Lukumay

Aidha, Dkt. Lukumay amesema mafanikio hayo yatakwenda sambamba na kuongeza ajira kwa vijana, kukuza uchumi wa viwanda na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni yanayotumika katika uagizaji wa dawa kutoka nje ya nchi.

Pia, Dkt. Lukumay amesema ongezeko la ushirikiano kati ya Serikali na wawekezaji wa kimataifa kutoka Marekani, Uingereza, India, Ujerumani na China, akisema hatua hiyo ni ushahidi wa mwamko mkubwa wa uwekezaji katika sekta ya uzalishaji wa dawa na vifaa tiba nchini.

Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe  amesema mafanikio ya uwekezaji katika Viwanda vya Dawa na vifaa tiba nchini yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, sekta binafsi, wataalamu pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kurahisha upatikanaji wa bidhaa hizo nchini. 

"Matokeo yanayoonekana sasa katika sekta ya Afya ni matunda ya kazi kubwa iliyofanywa na 'Pharmaceutical Industrial Acceleration and Facilitation Taskforce' (PIAT), kamati iliyoundwa mahsusi kwa ajili ya kuharakisha uwekezaji katika sekta ya afya," amesema Dkt. Shekalaghe 

Amesema kupitia kamati hiyo, Serikali imefanikiwa kuwakutanisha wadau mbalimbali ili kuhakikisha maamuzi yanafanyika kwa haraka na miradi ya uwekezaji inatekelezwa kwa ufanisi mkubwa.

Aidha, Dkt. Shekalaghe amewapongeza Viongozi na Wataalamu wanaoshiriki katika utekelezaji wa miradi hiyo kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi na kujituma kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya afya nchini.

Aidha, Dkt. Shekalaghe amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuboresha mifumo ya kazi na kuondoa changamoto zinazoweza kuchelewesha utekelezaji wa miradi ya uwekezaji katika sekta ya dawa na vifaa tiba.

"Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha uzalishaji wa dawa, chanjo na vifaa tiba kwa ajili ya soko la ndani na nchi nyingine za Afrika," amesema Dkt. Shekalaghe .

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »