KAMISHNA KUJI AZINDUA MRADI WA KUSAFIRISHA NA KUSAMBAZA UMEME KATIKA HIFADHI YA TAIFA MIKUMI

May 11, 2026


Na. Philipo Hassan - Mikumi

Mwisho mwa wiki ikiyopita, Kamishna wa Uhifadhi TANAPA CPA Musa Nassoro Kuji alizindua rasmi mradi wa kusafirisha na kusambaza umeme wa TANESCO ndani Hifadhi ya Taifa Mikumi. Mradi huo unaolenga kuboresha utoaji wa huduma ndani ya hifadhi, kuimarisha shughuli za uhifadhi na utalii, kuboresha matumizi ya nishati ya umeme kwa watumishi wa hifadhi na kuongeza fursa za uwekezaji katika sekta ya utalii.

Usambazaji wa umeme wa TANESCO ndani ya hifadhi utaboresha na kuleta mapinduzi makubwa kwenye upatikanaji wa nishati hiyo kwa watumishi, watalii, wawekezaji waliopo ndani ya hifadhi hiyo pamoja na wananchi ambao nao wamefaidika na umeme huo ambao pia umepita kwenye maeneo yao wakati wa utekelezaji wa mradi huo.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Menenejimenti ya hifadhi, Maafisa na Askari wa uhifadhi wakiongozwa na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Augustine Masesa ambaye ndiye Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mikumi, Meneja wa TANESCO Morogoro Kusini Mhandisi Lugata Masingija pamoja na wananchi wa maeneo jirani na hifadhi hiyo.

Kamishna Kuji aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuidhinisha bajeti ya mradi huo pia Bodi ya Wadhamini ya TANAPA kwa usimamizi wa karibu wa shughuli za Shirika ikiwemo utekelezaji wa mradi huo.

Aidha, Kamishna Kuii aliupongeza uongozi wa TANESCO kwa utekelezaji wa mradi huo ambapo mbali na kuunga mkono jitihada za Serikali za uwepo wa nishati safi utaongeza kasi ya maendeleo kwa wananchi wa vijiji jirani vilivyonufaika na mradi huu,” alisema Kamishna Kuji.

Mradi huo unaweka historia mpya katika Hifadhi ya Taifa Mikumi kwa kuimarisha matumizi ya nishati safi na uhakika, hatua inayotarajiwa kuongeza ubora wa huduma, kuchochea uwekezaji wa utalii na kuendelea kufungua fursa za maendeleo kwa jamii zinazozunguka hifadhi hiyo.











Share this

Related Posts

Previous
Next Post »