
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Serikali imesema itaendelea kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa mafuta nchini licha ya changamoto za kimataifa zinazoathiri mnyororo wa usambazaji wa nishati hiyo , ikiwemo vita inayoendelea katika Ukanda wa Mashariki ya Kati.
Akizungumza bungeni jijini Dodoma wakati wa uwasilishaji wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2026/27 ,Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Deogratius Ndejembi, alisema kuwa Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa za mafuta ya petroli kwa uhakika.
“Sambamba na kuimarika kwa upatikanaji wa umeme, nchi yetu pia imeendelea kuwa na uhakika wa upatikanaji wa bidhaa za mafuta ya petroli licha ya changamoto za kimataifa zilizotokana na vita baina ya Marekani, Israel na Iran,” alisema Mhe. Ndejembi.
Alifafanua kuwa vita hiyo imesababisha athari kubwa katika usambazaji wa mafuta duniani, ikiwemo kufungwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz ambao hupitisha zaidi ya asilimia 20 ya mafuta yote duniani, pamoja na kuathiri miundombinu ya uzalishaji na uhifadhi wa mafuta.
“Hali hii imeathiri kwa kiasi kikubwa nchi za Mashariki ya Kati ambako Tanzania inaagiza takribani asilimia 59 ya mafuta yake, huku asilimia 41 ikitoka India ambayo nayo hutegemea mafuta ghafi kutoka ukanda huo huo,” aliongeza.
Kutokana na hali hiyo, Waziri Ndejembi alisema Serikali imechukua hatua za haraka na za kimkakati ili kulinda usalama wa nishati nchini. Moja ya hatua hizo ni kuliwezesha Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuagiza mafuta ya kutosha kwa kipindi cha miezi mitatu ijayo.
Aidha, alisema Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa soko la mafuta duniani na iko tayari kuchukua hatua zaidi kulingana na mabadiliko yatakayotokea.

EmoticonEmoticon