Njombe Yaweka Rekodi ya Ubora katika Usimamizi wa Taka na Usafi wa Jamii

April 23, 2026
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekabidhi tuzo kwa Mkoa wa Njombe ikiwa ni Mshindi wa Jumla wa Shindano la Afya na Usafi wa Mazingira kwa Mwaka 2024.

Tuzo hiyo imekabidhiwa na Mgeni Rasmi wa Mkutano Maalum wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa ambaye ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba Aprili 22, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Arusha (AICC).

Akimkabidhi Tuzo hiyo Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI, Mhe. Profesa Riziki Silas Shemdoe amesema tuzo hiyo imetolewa na NEMC kwa kuthamini mchango wa Mkoa wa Njombe katika Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira.

Akizungumza na baadhi ya Waheshimiwa Wenyeviti na Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Njombe mara baada ya zoezi hilo la utoaji wa Tuzo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi amewapongeza kwa kuchukulia suala la Mazingira kwa umuhimu mkubwa na kutoa rai kwa Halmashauri nyingine Nchi nzima kuiga mfano wa Mkoa wa Njombe.

Akitoa neno la Shukrani kwa niaba ya Mkoa wa Njombe, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Makete, Mhe. Rabson A. Mahenge ameishukuru NEMC kwa kuthamini mchango wao katika kutunza mazingira na amesisitiza kuwa NEMC iendelee kutoa maelekezo Mkoa wa Njombe utatekeleza na matokeo yataonekana.

Wizara ya Afya kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo NEMC huendesha mashindano ya Afya na Usafi wa Mazingira kila mwaka. Mwaka 2024, na miaka mingine Mkoa wa Njombe umekuwa kinara katika uimarishaji wa huduma za usafi wa Mazingira.

Mkoa huo umekuwa ukiongoza kwa kuwa na kaya zenye vyoo bora, usafi wa mazingira na usafi binafsi katika ngazi ya kaya, Shule na Vituo vya kutolea huduma za afya.

Aidha, mkoa umekuwa mfano na darasa kujifunza kwa Halmashauri nyingine katika masuala ya udhibiti wa taka ngumu na maji taka.

Hali hii ya Mkoa inachangiwa na viongozi ngazi zote kuamua pamoja na wananchi kuyapa kipaumbele masuala ya usafi wa mazingira, hali inayochangia Mkoa kutopata visa vya ugonjwa wa kipindipundu kwa muda mrefu na wananchi kuendelea kujishughulisha na shughuli za kiuchumi.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »