JK AZINDUA HARAMBEE KUCHANGIA UJENZI WA MAABARA YA TEHAMA YA “DARASA JANJA” SHULE YA SEKONDARI KIBAHA

April 16, 2026





Na Issa Michuzi,

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Jumatano, Aprili 15, 2026, amehudhuria Mahafali ya 59 ya Shule ya Sekondari Kibaha (KSS) kama mgeni rasmi, katika hafla iliyofanyika shuleni hapo, Tumbi, Kibaha Mji, mkoani Pwani.

Akiwa katika mahafali hayo, Dkt. Kikwete amezindua harambee ya kuchangia ujenzi wa jengo la ghorofa la maabara ya TEHAMA na masomo mengine, ambalo linatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 3.

Amesema ujenzi huo ni muhimu katika kuendeleza ubunifu na uwezo wa wanafunzi katika masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM).

Aidha, Dkt. Kikwete amekubali kuwa mlezi wa kamati ya kukusanya michango kwa ajili ya mradi huo mkubwa ambao kwa sasa umefikia hatua ya msingi.


Pia, Rais Mstaafu ameishukuru jumuiya ya wanafunzi wa zamani (alumni) wa shule hiyo, wakiuongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Bw. Abdul Mombokaleo, kwa kuchangia kompyuta zenye thamani ya Shilingi Milioni 170 kwa ajili ya “Darasa Janja” (Smart Class) lililoanzishwa shuleni hapo.

Darasa hilo litakuwa ni kituo cha mafunzo kwa wanafunzi wa shule hiyo na shule nyingine zitakazounganishwa kupitia mfumo wa mtandao, ambapo mwalimu anaweza kufundisha madarasa yaliyoko nje ya Kibaha kwa wakati mmoja kwa njia ya kidigitali.

Katika ziara yake, Dkt. Kikwete alipata fursa ya kutembelea na kukagua Darasa Janja hilo, akipokea maelezo kutoka kwa Mkuu wa Shule kuhusu namna teknolojia hiyo inavyotumika kuboresha mbinu za ufundishaji na ujifunzaji shuleni hapo.

Shule ya Sekondari Kibaha, inayomilikiwa na Shirika la Elimu Kibaha na kusimamiwa na Kurugenzi ya Hud uma za Elimu, ilianzishwa mwaka 1965 kupitia ushirikiano kati ya Serikali ya Tanganyika ya wakati huo na nchi za Nordic – Denmark, Finland, Norway, na Sweden. Wakati inaanzishwa, shule ilikuwa na wanafunzi 110 wa Kidato cha Kwanza na 60 wa Kidato cha Tano.

Kwa sasa, shule hiyo ya bweni kwa wavulana ina uwezo wa kuchukua zaidi ya wanafunzi 800 na imeendelea kuwa miongoni mwa taasisi kongwe na zenye heshima kubwa katika sekta ya elimu nchini.

Dkt. Kikwete ni miongoni mwa alumni mashuhuri wa Shule ya Sekondari Kibaha, alikosoma zaidi ya miaka 60 iliyopita. Wengine waliopitia shule hiyo ni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mkurugenzi Mkuu wa ATCL Bw. Peter Ulanga, Balozi Lazaro Nyalandu, Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO Nchini Prof. Hamisi Malebo, Mkurugenzi Mkuu wa Viwanja vya Ndege Bw. Abdul Mombokaleo, na Mwenyekiti Mstaafu wa CHADEMA Mhe. Freeman Mbowe, miongoni mwa wengine wengi.

Aidha, kwa kutambua mchango mkubwa wa alumni wake, Shule ya Sekondari Kibaha inaendelea kuimarisha ushirikiano na wadau wa elimu ili kuhakikisha inaendelea kuwa kinara katika utoaji wa elimu ya ubora nchini.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Jumatano, Aprili 15, 2026, akikagua na kupewa maelezo juu ya maabara ya TEHAMA ambayoni ‘Smart Class” na Mkuu wa Shule hiyo alipokuwa Mgeni rasmi katika n Mahafali ya 59 ya Shule ya Sekondari Kibaha (KSS) kama mgeni rasmi, katika hafla iliyofanyika shuleni hapo, Tumbi, Kibaha Mji, mkoani Pwani.
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Jumatano, Aprili 15, 2026, akimpongeza na kumshukuru Mkurugenzi Mkuu wa Viwanja vya Ndege (TAA) Bw. Abdul Mombokaleo kwa kujitolea computer zenye thamani ya shilingi milioni 170 kama mchango wake yeye na Alumni wengine kwa kuboresha elimu ya Sayansi katika shule hiyo.
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Jumatano, Aprili 15, 2026, akupewa maelezo juu ya mradi wa jengo la maabara ya TEHAMA ambayo ni ‘Smart Class’ alipokuwa Mgeni rasmi katika Mahafali ya 59 ya Shule ya Sekondari Kibaha (KSS) kama mgeni rasmi, katika hafla iliyofanyika shuleni hapo, Tumbi, Kibaha Mji, mkoani Pwani.
Sehemu ya wahitimu wa kidato cha sita katika Mahafali ya 59 ya Shule ya Sekondari Kibaha (K katika hafla iliyofanyika shuleni hapo, Tumbi, Kibaha Mji, mkoani Pwani.
(Picha na Habari na Issa Michuzi)

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »