Operesheni hiyo iliyofanyika usiku wa kuamkia Aprili 14, 2026 katika ufukwe wa Magambani, eneo la Kaole Ufundi, ilifanikisha kukamatwa kwa viroba 18 vyenye jumla ya paketi 1,062 za mirungi. Katika tukio hilo, watuhumiwa wanne walikamatwa.
Akizungumza na waandishi wa habari Bagamoyo mkoani Pwani, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amewataja waliokamatwa kuwa ni Jamal Ally Faki (35) Shari Omary Salim (28), wote wakazi wa Tanga, Sebastian Protas Shirima (28) mkazi wa Temeke na James Michael Kimaro (27) mkazi wa Buza Dar es Salaam.
“Boti hii imekuwa ikitumika kwa muda mrefu kusafirisha mirungi kwa njia ya bahari kutoka Mombasa kuja Dar es Salaam na tumekuwa tukiifuatilia kwa muda mrefu, taarifa tuliyoitoa hivi karibuni tulieleza kwamba, mirungi imekamatwa kwa wingi kuliko dawa nyingine za kulevya, boti hii ndiyo iliyokuwa inaleta dawa hizo nchini. Na baada ya kuikamata tutakuwa tumedhoofisha mtandao wa usafirishaji wa dawa za kulevya hapa nchini” amesema Kamishna Lyimo.
Ameeleza kuwa, mabadiliko ya mbinu za usafirishaji yamejitokeza kufuatia kuimarika kwa operesheni dhidi ya dawa nyingine hatari kama heroin, cocaine, methamphetamine na skanka, pamoja na operesheni za kuteketeza mirungi Same, hali ambayo imesababisha wahalifu kuhamia kwenye mirungi inayosafirishwa kutoka Kenya.
Aidha, amesema Mamlaka inaendelea na operesheni endelevu za kudhibiti uzalishaji na usambazaji wa dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na kuteketeza mashamba ya bangi na kufuatilia mitandao mipya ya usafirishaji, huku akitoa wito kwa wananchi kushirikiana kwa karibu na Mamlaka kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kukomesha biashara hiyo haramu.
“Serikali iko makini kuhakikisha inadhibiti kabisa uingiaji wa dawa za kulevya nchini, na tutachukua hatua kali dhidi ya yeyote anayejihusisha na biashara hii,” amesema .
Kwa upande wake balozi wa shina namba moja katika kitongoji cha Kaole Ufundi, Dominic Masika ameipongeza Serikali kwa hatua nzuri walizochukua katika kukabiliana na dawa za kulevya.
“Tukio hili lililotokea hapa Kaole, Magambani linaonesha nia ya dhati ya Serikali katika kulinda usalama wa wananchi. Naiomba serikali iendelee kufanya operesheni kama hizi, kufanya doria za mara kwa mara na kuwekeza katika maeneo kama haya yenye vichaka kwani yanaweza kutumika vibaya kama sehemu za kupitisha dawa za kulevya,” amesisitiza.
Akizungumzia chanzo cha changamoto hiyo, ameeleza kuwa baadhi ya vijana wanajiingiza katika vitendo hivyo kutokana na kukosa uelewa sahihi, licha ya malezi na miongozo wanayoipata kutoka kwa wazazi. Hivyo, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wazazi, serikali na viongozi wa mitaa katika kupambana na tatizo la dawa za kulevya.





EmoticonEmoticon