Afisa Utamaduni wa Manispaa ya Kahama, Martha Kapela akizungumza na wanawake juu ya majukumu ya wanawake katika malezi, elimu ya maadili, na utunzaji wa familia huku akiwahimiza walimu kushirikiana katika malezi ya watoto shuleni.
Na Neema Nkumbi, Kahama
Afisa Utamaduni wa Manispaa ya Kahama, Martha Kapela, amesema mwanamke ndiye chanzo cha maadili katika jamii, huku akieleza kwamba yeye ndiye mlezi na msimamizi wa kwanza wa maadili nyumbani.
Akizungumza leo Machi 7, 2026 katika kongamano la wanawake lililofanyika Manispaa ya Kahama, amesema kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayoadhimishwa kila mwaka Machi 8, Kapela amesema: "Kila jamii inategemea mwanamke kueneza maadili mema kwa familia na watoto, Hivyo wanawake tunawajibika kulinda maadili, hususan katika familia zetu kwani tuna nafasi muhimu katika kujenga jamii yenye tabia bora."
Afisa huyo amebainisha kuwa maadhimisho ya siku hii yanatoa fursa kwa jamii kutambua mchango mkubwa wa wanawake katika malezi, elimu ya maadili, na utunzaji wa familia huku akiwahimiza waalimu kushirikiana katika malezi ya watoto shuleni.
"Ni jukumu letu sote kuheshimu, kuthamini, na kuunga mkono jukumu la mwanamke katika malezi na maadili, Walimu pia mtusaidie katika malezi pindi watoto wakiwa shuleni, ili kujenga taifa lenye maadili, tamaduni, na desturi zetu,"amesema Kapela.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Kahama, Joachim Simbila, amesema kuwa mtu anapomdharau mwanamke, hajitambui huku akisisitiza kuwa ni wajibu wa kila mtu kumtunza mama na si kumdharau, kwa sababu bila mama hakuna mtu angefika pale alipo sasa.
Naye Mwalimu Pili Joram kutoka Maswa Mkoani Simiyu, ambaye amehudhuria kongamano hilo, amesema wanawake wana jukumu kubwa la malezi katika familia kwani wakikosea tu familia inaharibika hivyo kila mama anatakiwa kujitambua katika kulinda maadili ya watoto na jamii kwa ujumla katika malezi huku wakimtegemea Mungu kwani bila Mungu watoto wataharibika," ameongeza.
Aidha, Sharifa Salumu kutoka Manispaa ya Kahama, amezungumzia changamoto ya vijana kutokuwa na maadili, ambapo amebainisha kuwa Mmomonyoko wa maadili mizizi yake ipo nyumbani kwani kijana akipata malezi mazuri, hawezi kupotoshwa hivyo Vijana wakijitambua na kujielewa, hawatapotoshwa na teknolojia bali wataishi kwa maadili na mila za Kitanzania.
Kauli mbiu katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu ni: "Haki kwa wanawake na wasichana ni msingi wa maendeleo jumuishi kufikia dira ya 2050."














EmoticonEmoticon