DC NYAMWESE: RAIS SAMIA ANAWATUA NDOO KICHWANI WANAWAKE WA HANDENI

March 08, 2026

Na Mwandishi Wetu

MKUU wa Wilaya ya Handeni, Salum Nyamwese, amesema Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuwatua ndoo kichwani wanawake wa Handeni kupitia utekelezaji wa mradi wa maji wa miji 28 ambao umefikia zaidi ya asilimia 75 ya utekelezaji.

Mradi huo unaogharimu Dola za Marekani 81,142,931 unatekelezwa na mkandarasi M/s Jwil Infra Limited kutoka India na unatarajiwa kuhudumia zaidi ya wakazi 870,629 kutoka vijiji 161 vya wilaya za Handeni, Korogwe, Muheza na Pangani.

Nyamwese ametoa kauli hiyo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika Halmashauri ya Mji Handeni chini ya kaulimbiu isemayo “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana; Msingi Jumuishi kufikia Dira 2050.”

Amesema mradi huo utakuwa mkombozi kwa wanawake ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitumia muda mwingi kutafuta maji.

“Niwahakikishie msikae kinyonge mkajiona nyie ni dhaifu. Serikali imewasikia na tatizo hili la maji litatatuliwa hivi karibuni… hata yale mnayosema kina mama wanashindwa kusuka nywele vizuri kwa sababu ya maji, watasuka na tutawaona,” amesema.

Nyamwese amesema serikali chini ya uongozi wa Rais Samia imeendelea kuweka mazingira rafiki ya kumuwezesha mwanamke kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo kupitia sera, sheria na mipango mbalimbali.

Amebainisha kuwa Rais Samia pia alitoa maelekezo ya kuboreshwa kwa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu baada ya kubaini awali kulikuwa na changamoto katika utoaji wake.

“Mheshimiwa Rais alielekeza halmashauri kuweka utaratibu mzuri wa utoaji wa mikopo hii ili kuhakikisha makundi haya yanapata fursa ya kujikwamua kiuchumi,” amesema.

Ameongeza kuwa Wilaya ya Handeni imeendelea kushuhudia maendeleo ya wanawake katika shughuli za kiuchumi zikiwamo ujasiriamali, kilimo na ufugaji.

Kuhusu kupambana na ukatili wa kijinsia, Nyamwese amesema serikali inaendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuheshimu utu wa mwanamke na kumpa mtoto wa kike nafasi sawa katika fursa mbalimbali.

“Changamoto ya ndoa za utotoni, mimba za utotoni na mila potofu zinazokwamisha maendeleo ya mwanamke, ikiwamo umiliki wa ardhi, serikali imeendelea kuzishughulikia,” amesema.

Amewataka viongozi wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi la Halmashauri ya Mji Handeni kuandaa mpango maalum wa kutoa elimu kwa wanawake ili kuwajengea uwezo wa kutumia fursa zilizopo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni, Maryam Ukwaju, amesema halmashauri imejipanga kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi ili kufikia malengo ya Dira 2050.

Amesema hadi mwisho wa Machi 2026 halmashauri inalenga kusajili angalau vikundi 50 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika mfumo wa NEST ili vinufaike na miradi inayotekelezwa katika eneo hilo.

Awali akisoma risala ya wanawake wa halmashauri hiyo, Carin Umwambe, amesema ukosefu wa maji umekuwa ukisababisha wanawake kutumia muda mwingi kutafuta maji badala ya kujishughulisha na shughuli za maendeleo na kuiomba serikali kuharakisha upatikanaji wa huduma hiyo.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »