
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam, Machi 10, 2026. Tume ya Ushindani (FCC) imesema itaendelea kusimamia kwa karibu haki za walaji kwa taasisi na kampuni zinazotumia mikataba iliyoandaliwa kwa upande mmoja, ili kuhakikisha watumiaji wa huduma na bidhaa hawapati hasara kutokana na mikataba hiyo.
Kauli hiyo imetolewa leo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa, alipokuwa akizungumza katika semina ya wadau kutoka taasisi na kampuni zinazotumia mikataba ya upande mmoja, iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Ngasongwa alisema FCC inaendelea kufuatilia kwa karibu mikataba ya aina hiyo ili kuhakikisha haikiuki haki za walaji katika soko. Alifafanua kuwa mikataba ya upande mmoja hutumiwa sana na taasisi mbalimbali kwa lengo la kurahisisha utoaji wa huduma kwa wakati, lakini ni muhimu iwe chini ya uangalizi ili kuepuka matumizi yanayoweza kuwa kinyume na sheria za ushindani na ulinzi wa mlaji.
Alisema semina hiyo ni sehemu ya mwendelezo wa utoaji wa elimu kwa wadau kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mlaji Duniani, yanayolenga kuongeza uelewa kuhusu haki na wajibu wa walaji pamoja na watoa huduma.
“Ninatambua kuwa mikataba inayoandaliwa kwa upande mmoja ina faida katika kurahisisha utoaji wa huduma kwa wakati. Hata hivyo, FCC ina jukumu la kuifuatilia kwa karibu, kwani bila uangalizi kunaweza kuwa na mambo yanayofanyika kinyume na maslahi ya walaji katika soko,” alisema Ngasongwa.
Aliongeza kuwa hata pale taasisi zinapotaka kuunganisha huduma au mikataba yao, ni muhimu kufanya tathmini ya kina ili kubaini kama kuna vipengele vinavyoweza kukiuka masharti ya ushindani au kuathiri ubora wa huduma kwa walaji.
Ngasongwa alisisitiza kuwa kila mtu ni mlaji kwa namna moja au nyingine, hivyo ni muhimu kuhakikisha thamani ya fedha inayotolewa na mteja inaendana na ubora wa huduma au bidhaa anayopata. Alisema hali hiyo pia husaidia kujenga uaminifu kati ya watoa huduma na walaji.
Aidha, alisema FCC itaendelea kukutana na makundi mbalimbali ya wadau kwa lengo la kuwapa uelewa mpana kuhusu majukumu ya taasisi hiyo na umuhimu wa kuzingatia sheria za ushindani na ulinzi wa mlaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA), Tusekelege Mwaikasu, alisema semina hiyo ni muhimu kwa taasisi za kifedha kwani itawasaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa walaji kwa kuzingatia viwango vinavyokubalika.
Alisema benki, kupitia umoja wao, zimekuwa zikitekeleza kampeni ya “Niko Fiti”, inayolenga kuhakikisha huduma za kifedha zinatolewa kwa ubora na kwa kuzingatia mahitaji ya walaji.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindqni Ushindani Ushindani (FCC), Bi. Khadija Ngasongwa akizungumza wakati akifungua Semina kwa Taasisi na Kampuni zenye mikataba iliyoandaliwa upande mmoja jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Udhibiti wa Mienendo ya Bidhaa inayokatazwa na Sheria ya Ushindani FCC, Bi.Magdalena Utouh akizunguza wakati wa kuhitimisha semina ya wadau wa Taasisi na Kampuni zenye mikataba iliyoandaliwa na upande mmoja jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa FCC,Bi. Roberta Feruzi akitoa maelezo kuhusiana na Semina ya wadau wa Taasisi na Kampuni zenye mikataba iliyoandaliwa upande mmoja jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA ) Bi.Tusekelege Mwaikasu akitoa neno kwa niaba ya wadau katika mkutano na FCC ,jijini Dar es Salaam.
Mkutano ukiendelea
Kaimu Mkurugenzi Mkurugenzi Mkuu wa FCC Khadija Ngasongwa akiwa katika matukio picha za za pamoja makundi mbalimbali.

EmoticonEmoticon