SHULE 13 TEMEKE KUANZA KUPIKA KWA UMEME

March 10, 2026




Na Mwandishi Wetu


GHARAMA za kupika chakula cha wanafunzi katika shule 13 za msingi Wilaya ya Temeke, mkoani Dar es Salaam, zinatarajiwa kupungua kwa kiasi kikubwa kufuatia shule hizo kuanza kutumia nishati ya umeme kupikia badala ya kuni.


Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa majiko ya umeme katika taasisi za elimu ya msingi unaosimamiwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Nishati, Idara ya Elimu ya Awali na Msingi ya Wilaya ya Temeke pamoja na Shirika la Chakula Duniani (WFP).

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi huo katika Shule ya Msingi Kibasila, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Halima Rukumbwe, amesema awali walikuwa wanatumia kati ya Sh.20,000 hadi Sh.25,000 kwa siku kupika chakula cha wanafunzi 450, ikiwemo uji na chai ya asubuhi pamoja na chakula cha mchana cha wali na maharagwe.

Amesema baada ya kuanza kutumia majiko ya umeme, gharama hizo zimepungua na kufikia kati ya Sh.8,000 hadi Sh.10,000 kwa siku, huku kiasi hicho kikijumuisha pia matumizi ya mota ya kupandisha maji kwa shughuli mbalimbali za shule.

“Mbali na kupunguza gharama, wapishi sasa wanapika chakula kwa muda mfupi zaidi na katika mazingira safi,” amesema Rukumbwe.


Ameongeza kuwa matumizi ya nishati hiyo yamechangia pia kupungua kwa utoro wa wanafunzi, kwani chakula kinapatikana kwa wakati na hivyo kuwahamasisha wanafunzi kuhudhuria masomo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia wa Wizara ya Nishati, Omar Khalifa amesema mradi huo katika awamu ya kwanza unatekelezwa katika mikoa minne ambayo ni Dar es Salaam (Wilaya ya Temeke), Dodoma (Wilaya ya Dodoma Mjini), Tabora (Wilaya ya Tabora Mjini) na Kigoma.

Naye, Mshauri wa Chakula kutoka Shirika la Chakula Duniani (WFP), Dkt. Geoffrey Ngegwa amesema katika Mkoa wa Dar es Salaam mradi huo unatekelezwa katika shule 13 za Wilaya ya Temeke.

Amesema mbali na Shule ya Msingi Kibasila ambayo tayari imeanza kutumia mfumo huo, shule nyingine zinazoendelea kukamilishiwa miundombinu ni Likwati, Madenge, Umoja, Alhasan Mwinyi, Unubini, Lioness Miburani, Nzasa, Ponde, Wailes, Chemchem na Charambe.

Ameongeza kuwa miundombinu katika shule hizo tayari imekamilika na kinachosubiriwa kwa sasa ni ufungaji wa masufuria ya kisasa ya kupikia (pressure cooker) unaotarajiwa kukamilika mwishoni mwa Machi 2026.


&&&

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »