MRAJIS AAGIZA MATUMIZI YA MIZANI ZA KIDIGITALI KULINDA WAKULIMA.

March 24, 2026

Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege amevitaka Vyama vya Ushirika vya Mazao nchini kutumia mizani za kidigitali katika kupima mazao ya wakulima ili kuondoa udanganyifu na kumlinda mkulima. Mrajis ametoa maelekezo hayo kupitia barua ya tarehe 13 Machi, 2026 aliyowaandikia Wenyeviti na Wajumbe wa Bodi wa Vyama vya Ushirika vya mazao Tanzania Bara kuhakikisha kuwa vinatumia mizani za kidigitali kwa lengo la kuondoa udanganyifu kwenye upimaji wa mazao ya wakulima na kurahisisha upatikanaji wa takwimu sahihi za makusanyo/mauzo ya mazao. Vyama vya Ushirika wa Mazao vitakavyobainika kuwa na Mizani ya kidijitali na havitumii Mizani hizo au kuzitumia kwa matumizi tofauti na malengo yaliyokusudiwa, vitachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria; na wakulima wanatakiwa kuhakikisha mazao yao yanapimwa kwa kutumia Mizani zilizounganishwa na Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU) ili kuwawezesha kupata malipo stahiki ya mazao yao. Aidha, Dkt. Ndiege amevitaka Vyama vyote vya Ushirika wa Mazao ambavyo bado havijatekeleza maelekezo ya ununuzi wa Mizani za kidijitali kuhakikisha kuwa vinanunua Mizani hizo kwa kufuata utaratibu wa manunuzi na Mwongozo wa Ofisi ya Mrajis kuhusu Ununuzi wa Mizani hadi kufikia Juni 31, 2026. Tume ya Maendeleo ya Ushirika inaendelea na jitihada za kuimarisha Usimamizi wa Vyama vya Ushirika nchini ambapo kwa sasa moja ya kipaumbele kinachotiliwa mkazo ni kuratibu na kuhimiza Vyama vya Ushirika vya Mazao, kuweka utaratibu wa ununuzi wa Mizani za Kidijitali sambamba na matumizi sahihi ya mizani hizo.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »