TFS YAJIPANGA KUIMARISHA HUDUMA KWA WANANCHI NA MAZINGIRA BORA YA KAZI KWA VIJANA

February 19, 2026

 

Morogoro, Februari 19, 2026 — Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo, amewataka viongozi na makamanda wa vituo vya wakala huo kubadili mtazamo wa uongozi kwa kusikiliza wananchi, kuwaelewa vijana wa ajira mpya na kusimamia migogoro ya rasilimali kwa busara, akisisitiza kuwa ofisi za umma hazina kisingizio cha kuchelewesha majibu kwa wananchi.

Akizungumza leo katika siku ya pili ya Mkutano wa Nne wa Viongozi na Makamanda wa Vituo vya TFS unaoendelea katika Ukumbi wa Hoteli ya Kate, Morogoro, Prof. Silayo alisema mabadiliko ya kijamii na kimazingira yanailazimu TFS kuwa na fikra pana zaidi na mbinu mpya za uongozi na utatuzi wa changamoto.

“Serikali imeweka mwelekeo wa kuwasikiliza wananchi. Hivyo, kila kiongozi wa TFS kwa nafasi yake anapaswa kuwa tayari kusikiliza, kujibu na kutatua changamoto zinazoletwa mezani. Ofisi ni ya Serikali; haijalishi ulikuwepo au hukuwepo wakati tatizo linaanza,” alisisitiza.

Prof. Silayo alisema TFS inapaswa kuendana na kasi ya mabadiliko ya kijamii yanayoathiri mitazamo ya vijana wanaoajiriwa sasa, akibainisha kuwa kizazi kipya kina matarajio tofauti kuhusu mazingira ya kazi.

“Leo kijana anaajiriwa akiwa tayari na matarajio maalum. Hatuwezi kuwachukulia kama wasikilizaji tu; tunapaswa kuwaheshimu, kuwaongoza na kuwajengea motisha,” alisema, akihimiza viongozi wa vituo kuwa tayari kupokea mawazo mapya na kuimarisha mazingira ya kazi yanayozingatia utu na heshima.

Akizungumzia athari za mabadiliko ya tabianchi na shinikizo la kijamii, Prof. Silayo alisema ongezeko la mahitaji ya rasilimali linaweza kuchochea migogoro kati ya wananchi na hifadhi, hivyo akawataka viongozi kusimamia hali hiyo kwa weledi.

Alitoa mfano wa baadhi ya wananchi wanaochoma misitu kwa lengo la kujikinga dhidi ya wanyamapori waharibifu, akisema hatua hizo ni matokeo ya “mikakati ya kuishi” inayotokana na msongo wa kimazingira.

“Hatuwezi kupuuza dalili hizi. Ni lazima tuwafikie wananchi, tuwasikilize na tushirikiane nao kabla madhara hayajawa makubwa,” alisema.

Alibainisha kuwa migogoro haiwezi kuepukika kabisa, bali kinachopaswa kusimamiwa ni kiwango chake na namna ya kuimudu kwa ustahimilivu na majadiliano ya wazi.

Kamishna alisisitiza umuhimu wa kushirikiana na mamlaka za wilaya, mikoa pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama katika operesheni na doria maalum, akisema ushirikiano huo husaidia taasisi kuwa na sauti na ulinzi mpana hata pale maofisa wake wanapokosekana.

Alionya dhidi ya tabia ya kuahirisha utekelezaji wa maazimio ya mikutano, akitaka kila azimio liwe na majibu na hatua za utekelezaji kwa wakati.

“Haiwezekani tuwe na azimio la mwaka mzima halafu leo hatuna jibu. Tatizo linaweza kuwa la mfumo, lakini lisiwe la uzembe wa utendaji,” alionya.

Mkutano huo wa siku tano unajadili utekelezaji wa maazimio ya mwaka uliopita, changamoto za kiutendaji katika vituo vya TFS na mikakati ya kuimarisha uhifadhi endelevu wa misitu na nyuki sambamba na kushirikisha michezo (TFS Bonanza) ambayo vyote vimepewa kaulimbiu ya “One Team, One Dream”.

Akihitimisha hotuba yake, Prof. Silayo alitangaza rasmi kuanza kwa shughuli za siku ya pili ya mkutano huo, akiwataka viongozi hao kutumia fursa hiyo kubadilishana uzoefu na kuimarisha mshikamano katika kusimamia rasilimali za misitu kwa manufaa ya taifa.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »