SIKU 100 ZA RAIS SAMIA: BILIONI 69 ZA REA KUNUFAISHA VITONGOJI 634 MKOANI RUVUMA

February 03, 2026
-Mradi unatekelezwa kwa Miaka Mitatu

Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza mradi kabambe wa shilingi bilioni 69 wa kusambaza umeme katika vitongoji 634 utakaonufaisha wateja wa awali 20,328 Mkoani Ruvuma.

Meneja Usimamizi wa Miradi ya Kusambaza Umeme wa REA, Mhandisi Deogratius Nagu amebainisha hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy Februari 02, 2026 Mkoani Ruvuma wakati wa kuwatambulisha Wakandarasi watakaotekeleza mradi Kampuni ya mzawa ya Energy Services Ltd na Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Kusafirisha na Kusambaza Umeme (ETDCO) kwa Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Brigedia Jenerali Ahmed Abasi Ahmed.

“Tunamshukuru Rais Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kiasi cha shilingi 69,134,982,657.9576 kitumike kusambaza umeme katika vitongoji 634 mkoani hapa na leo hii tumefika hapa kuwatambulisha wakandarasi na maandalizi ya awali ya kutekeleza mradi yameanza,” amesema Mhandisi Nagu.

Akizungumza wakati wa utambulisho wa wakandarasi hao, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Ahmed ameipongeza REA kwa kuendelea kutekeleza dhamira na maono ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa vitendo na kuwataka wakandarasi hao kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na ubora unaotakiwa.

Amesema umeme unakwenda kuongeza chachu ya maendeleo na kuimarisha huduma za kijamii na kiuchumi na ametoa wito kwa wananchi maeneo ya mradi kuchangamkia fursa zitokanazo na mradi lakini pia kuwa waadilifu kwa kulinda na kutunza miundombinu ya umeme na pia kuwapatia ushirikiano wakandarasi.

“Tuwahakikishie Mkoa unao wataalam walio tayari kufanya kazi muda wowote, hivyo tunawahakikishia ushirikiano wa kutosha na ni wajibu wetu kuhakikisha ulinzi na usalama lakini pia wakandarasi mnapaswa kuwa waadilifu na mjikague wenyewe kwa wenyewe,” ameelekeza Brigedia Ahmed.

Akizungumzia hali ya usambazaji umeme mkoani humo, Mhandisi Nagu amesema kuwa vijiji vyote 551 vimefikishiwa umeme na kwamba hadi sasa vitongoji 2,107 vimefikishiwa umeme kati ya vitongoji 3,691 na kwamba kazi inaendelea ya kusambaza umeme katika vitongoji 731.

Mha. Nagu amefafanua kuwa ETDCO atatekeleza mradi kwenye vitongoji 262 katika Wilaya za Mbinga na Nyasa kwa gharama ya shilingi bilioni 37.9 na huku Energy Services akitekeleza kwenye vitongoji 372 kwa gharama ya shilingi bilioni 31.2 katika Wilaya za Songea, Namtumbo na Tunduru

Amesema, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 vitongoji vyote nchini viwe vimefikishiwa nishati ya umeme na kwamba REA ikiwa na dhamana hiyo imejipanga kikamilifu kupitia miradi mbalimbali ya kimkakati kufikia dhamira hiyo.

Pia, Mhandisi Nagu amesema mradi unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu na ameiomba Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kushirikiana na REA kufikisha elimu na taarifa sahihi kwa wananchi sambamba na kuhamasisha wananchi kuunganishiwa umeme.

Aidha, kwa upande wao wakandarasi wa mradi huo walimhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa watatekeleza mradi kwa uaminifu, uadilifu na uzalendo kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za Serikali.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »