Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, ameielekeza kampuni ya Abanyambo Enterprises & General Supplies Ltd kuendelea na shughuli za uchimbaji wa madini ya bauxite katika Kata ya Magamba, Wilaya ya Lushoto, mkoani Tanga.
Hatua hiyo imekuja kufuatia utekelezaji wa agizo lililokuwa limetolewa awali na Waziri Mkuu mstaafu, Kassim Majaliwa, ambaye alisitisha uchimbaji huo hadi tathmini ya athari kwa mazingira na binadamu itakapofanyika na kukamilika.
Akizungumza wakati wa ziara yake mkoani humo, Waziri Mkuu alisema kampuni hiyo, ambayo inamiliki leseni nne halali, imeruhusiwa kuendelea na uzalishaji baada ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kujiridhisha na kutoa kibali rasmi cha tathmini ya athari kwa mazingira.
Alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu swali la aliyekuwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Magamba, Mahamud Kotti, ambaye alitaka kujua msimamo wa Serikali kuhusu mradi huo. licha ya uchimbaji huo kuwa chanzo cha ajira na mapato kwa kijiji na halmashauri.
Hata hivyo Waziri Mkuu alisisitiza kuwa Serikali haitavumilia uvunjaji wa sheria katika sekta ya madini, akieleza kuwa wawekezaji wote wanapaswa kufuata taratibu zilizowekwa ili kulinda rasilimali za taifa pamoja na mazingira.
Katika hatua nyingine, alitangaza kusimamishwa kwa leseni 45 zilizokuwa zikitaka kufanya shughuli katika mgodi huo kinyume na sheria na masharti ya uchimbaji.
Alifafanua kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya kubainika kuwepo kwa ukiukwaji wa taratibu ambao ungeweza kuhatarisha usalama wa mazingira na kusababisha upotevu wa mapato ya Serikali.
“Hatutakuwa tayari kuona rasilimali za nchi zinachimbwa bila kufuata sheria. Lazima kila mmoja aheshimu utaratibu,” alisisitiza Waziri Mkuu.
Aidha, amemuagiza Afisa Madini Mkoa wa Tanga kusimamia kikamilifu utekelezaji wa agizo hilo na kuhakikisha kuwa kampuni ya Abanyambo pekee ndiyo inayoendelea na shughuli za uchimbaji katika eneo hilo.
Ziara hiyo ni sehemu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo na shughuli za kiuchumi unaofanywa na Waziri Mkuu, kwa lengo la kuhakikisha sheria, uwazi na uwajibikaji vinazingatiwa katika usimamizi wa rasilimali za taifa.


EmoticonEmoticon