📌Ni kuelekea asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034
📍Morogoro
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kutumia teknolojia mbalimbali ikiwemo matumizi ya mkaa mbadala unaozalishwa nchini ili kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034 kulingana na Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya nishati safi hapa nchini.
Wito huo umetolewa leo Februari 28, 2026 na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu akiwa ameongoza na Menejimenti ya REA wakati walipotembelea kiwanda cha Shirika la Mzinga kujionea kuhusu uzalishaji wa teknolojia ya mkaa mbadala unaofanywa na Shirika hilo mkoani Morogoro.
Balozi Meja Jenerali Mstaafu Kingu ameeleza kuwa Serikali kupitia REA imehamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia katika ajenda ya Kitaifa ya nishati safi ya kupikia katika kuwawezesha Watanzania wanatumia nishati hiyo ifikapo mwaka 2034.
"Matumizi ya mkaa mbadala yatatuwezesha kuweza kufikia asilimia 80 ya watanzania kutumia nishati safi ifikapo mwaka 2034. Ni lazima tuipe nguvu ajenda hii kwa kuwa inakwenda kuwa mkombozi kwa nchi yetu, " Ameongeza Balozi Kingu.
Kwa upande wake, Brigedia Jenerali Seif Hamisi ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mzinga ameishukuru REA kwa fursa hiyo ya kuwatembelea katika kiwanda chao cha Mzinga na kujionea namna uzalishaji wa mkaa mbadala unavyofanywa na kiwanda hicho mkoani humo.
Amesema, ni matarajio yao kuwa kiwanda hicho kinakwenda kukidhi mahitaji ya watumiaji wa mkaa mbadala kwa kuwa kwa sasa wanaendelea kufanya tafiti na kuzungumza na wadau mbalimbali ikiwemo REA ili kuhakikisha wanapata teknolojia za kisasa zitakazowezesha kuanza kuzalisha mkaa huo kwa wingi.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Mradi wa mkaa mbadala katika kiwanda cha Mzinga Mha. Amiri Msangi, ameeleza kuwa kwa sasa kiwanda kinaendekea kufanya tafiti wa teknolojia teknolojia bora na rafiki ya uzalishaji wa mkaa mbadala ili uzalishaji utakapoanza na kuwa mkubwa uweze kuleta tija kwa Watanzania na kuongeza kipato kwa shirika.
Mwisho.







EmoticonEmoticon