URAMBO NA KALIUA ZIPO TAYARI KWA UWEKEZAJI-WAZIRI NDEJEMBI

February 14, 2026


Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema wilaya za Urambo na Kaliua mkoani Tabora zipo tayari kwa uwekezaji, hususan wa viwanda kwani umeme unaopatikana katika Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme Urambo unatosheleza na hata kuzidi mahitaji ya sasa.

Amesema hayo leo, tarehe 14 Februari 2026, wakati akikagua mradi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa Kilovoti 132 kutoka Tabora hadi Urambo na Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Uhuru - Urambo cha Megawati 24.

“Urambo ipo tayari kwa uwekezaji. Uwezo wa kituo cha Urambo ni megawati 24, lakini matumizi ya wilaya mbili za Kaliua na Urambo ni megawati 2.5 wakati wa mchana na wakati wa usiku ambacho ni kipindi watu wengi wanakuwa majumbani, kiwango cha juu cha matumizi ni megawati 7,” amesisitiza Ndejembi.

Ndejembi amesema lengo na dhamira ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kunakuwa na nishati ya umeme ya uhakika ili kuendelea kuchochea uwekezaji katika maeneo yote nchini, kwani nishati ya umeme ni kichocheo cha sekta zote.

Amesema wilaya za Urambo na Kaliua zimejikita zaidi katika kilimo hususan zao la Tumbaku, zao ambalo linahitaji kuongezewa thamani kupitia viwanda vilivyokuwa vinahitaji umeme wa uhakika.

Aidha, Ndejembi amesisitiza kuwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tayari ametoa zaidi ya trilioni 1.9 kwa Wizara ya Nishati kupitia TANESCO kwa ajili ya Mradi wa Gridi Imara kujenga vituo vya kupoza na njia za kusafirisha umeme wa kutosha na wa uhakika katika maeneo mbalimbali nchini.

Kadhalika, Mhe. Ndejembi amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Urambo, Magreth Sitta ambaye alitoa eneo la hekari 20 lililotumika kujenga Kituo hicho cha Kupooza Umeme.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema mradi wa ujenzi wa Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme Urambo ulianza kutekelezwa Septemba 2021 kwa gharama ya shilingi bilioni 44. Kati ya hizo, bilioni 24 zilitumika kujenga njia ya kusafirisha umeme, bilioni 16 zimejenga kituo cha kupoza  na bilioni 4 ilitumika kufidia wananchi waliopitwa na mradi.

Twange amesema kituo hicho kilianza kufanya kazi mwezi Machi 2025, ambapo ujenzi wa njia ya umeme pamoja na kituo cha kupokea na kupooza umeme vyote vimekamalika kwa asilimia 100.



Share this

Related Posts

Previous
Next Post »