DC NYAMWESE ATAKA MASHAURI YA ARDHI YASIKILIZWE HARAKA KUCHOCHEA MAENDELEO HANDENI

February 02, 2026

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Salum Nyamwese,akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria yaliyofanyika katika Mahakama ya Wilaya ya Handeni leo Februari 2,2026.

Na Augusta Njoji

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Salum Nyamwese, ametoa rai kwa Mahakama ya Wilaya ya Handeni kutoa kipaumbele katika usikilizwaji wa mashauri yanayohusu ardhi ili yahitimishwe kwa wakati na kuchochea maendeleo ya wananchi.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria yaliyofanyika katika Mahakama ya Wilaya ya Handeni, Mhe. Nyamwese amesema migogoro ya ardhi imekuwa ikichukua muda mrefu kusikilizwa pindi inapofikishwa mahakamani, hali inayosababisha kucheleweshwa kwa utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

Amesema ardhi ni rasilimali muhimu katika Wilaya ya Handeni, lakini imeendelea kukumbwa na migogoro mingi, ambayo baadhi yake haina tija kwa maendeleo ya jamii.

Amesisitiza kuwa haki inapocheleweshwa, maendeleo nayo hucheleweshwa, hususan pale wananchi wanapokusudia kutumia ardhi kwa uwekezaji au shughuli za uzalishaji.

“Sisi kama Wilaya tumekuwa na migogoro ya ardhi, lakini inapofika mahakamani mashauri haya huchukua muda mrefu kusikilizwa. Hali hii inawaathiri wananchi na kudumaza maendeleo kwa ujumla,” amesema Mhe. Nyamwese.

Aidha, amepongeza hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha utendaji wa Mahakama, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya mahakama karibu na wananchi pamoja na matumizi ya teknolojia, hatua zinazoongeza imani ya wananchi katika mfumo wa utoaji haki.

Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Handeni, Joseph Waruku, amesema Mahakama imeendelea kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kuanzisha Mahakama za Mwanzo 12 mwaka 2025 katika maeneo yenye msongamano wa mashauri, ikiwemo Mahakama ya Mwanzo Msomera.

Naye, Mwakilishi wa Mwanasheria wa Halmashauri ya Mji Handeni, Regina Pangah, amesema Mahakama zina mchango mkubwa katika ustawi wa jamii na ukuaji wa uchumi kwa kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati, huku akiahidi kuendeleza ushirikiano katika kutoa elimu ya sheria kwa wananchi.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »