*📌Idadi ya vitongoji vyenye umeme Mbeya ni 1,970 sawa na asilimia 67%*
*📌Mkandarasi atakiwa kutekeleza mradi huo kulingana Taratibu zilizowekwa*
📍Mbeya
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Beno Malisa ameishukuru Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kwa kupeleka kiasi cha shilingi bilioni 42.6 mkoani Mbeya ili kupeleka umeme kwenye vitongoji 316 kupitia mradi wa HEP 2B unaotekelezwa mkoani humo ili wananchi wanufaike na nishati hiyo.
RC Malisa amesema mradi huo unakwenda kuleta tija na kuchochea maendeleo ya wananchi wa mkoa huo ambao wataunganishiwa umeme huo kuwawezesha kuendesha shughuli zao za kiuchumi.
"Gharama ya kuunganisha umeme ni shilingi 27,000 tu. Nawaomba wananchi wa mkoa huu mtumie fursa hii ya kuunganisha umeme iliyoletwa na Serikali kupitia REA.," Amesema RC Malisa.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa REA, Bw. Frank Mugogo amesema jumla ya Vitongoji mkoa wa Mbeya ni 2,951 ambapo vitongoji vyenye umeme ni 1,970 sawa na asilimia 67%.
Ameongeza kuwa vitongoji ambavyo havina umeme ni 1,981 na vitongoji vilivyopo kwenye mradi huo wa HEP 2B uliotambulishwa mkoani Mbeya ni 316 na vitongoji vitakavyosalia ni 665.
Kwa upande wake, Meneja wa Miradi kutoka kampuni ya White City International Contractors Ltd, Mha.Baraka Mungai ambaye atatekelesa mradi huo ameishukuru Serikali kupitia REA kwa kupewa fursa ya kutekeleza mradi huo. Ameuhakikishia uongozi wa mkoa wa Mbeya kuwa mradi huo utakamilika kwa wakati ili uweze kuleta tija kwa wananchi wa mkoa huo.






EmoticonEmoticon