TANZANIA YAIMARISHA UTAYARI WA KUKABILIANA NA TISHIO LA EBOLA

June 18, 2026

NA EMMANUEL MBATILO, DODOMA

SERIKALI imesema Tanzania bado haina mgonjwa wa Ebola na hali ya usalama wa afya nchini inaendelea kuwa nzuri, huku ikieleza kuwa imeimarisha hatua mbalimbali za kuzuia ugonjwa huo kuingia nchini kutokana na mlipuko unaoendelea katika nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Uganda.

Akitoa taarifa kwa umma kuhusu mwenendo wa tishio la ugonjwa wa Ebola na hatua zinazochukuliwa kuimarisha utayari wa taifa, Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa amesema Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha ugonjwa huo hauingii nchini kupitia mifumo madhubuti ya ufuatiliaji, utambuzi na udhibiti wa magonjwa.

Mchengerwa amesema tangu kutangazwa kwa mlipuko huo mwezi Mei mwaka huu, Serikali imeendelea kutekeleza hatua za kinga na udhibiti ikiwemo kutoa Mwongozo wa Wasafiri (Travel Advisory) Na.17 wa Mei 19, 2026 unaobainisha tahadhari kwa wasafiri wote wanaoingia nchini.

Amesema ufuatiliaji wa tetesi za Ebola umeimarishwa katika jamii na maeneo ya mipakani, ambapo hadi sasa jumla ya tetesi 64 kutoka mikoa 21 zimeripotiwa. Kati ya hizo, wahisiwa 11 walikidhi vigezo vya uchunguzi, walichukuliwa sampuli na baada ya vipimo kuthibitika kutokuwa na maambukizi ya Ebola.

“Mpaka sasa nchi yetu haina mgonjwa wa Ebola na hali ya usalama wa afya nchini iko vizuri. Hata hivyo, Serikali inaendelea kuchukua hatua za mapema na za kina ili kuhakikisha ugonjwa huu hauingii nchini,” amesema Waziri Mchengerwa.

Aidha, amesema Serikali imeimarisha utayari wa wataalamu wa afya na vituo vya kutolea huduma nchini kwa kuhakikisha upatikanaji wa dawa, vifaa kinga na vifaa tiba muhimu kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo endapo utatokea.

Pamoja na hayo amesema seti za kutosha za vifaa maalumu vya kujikinga zinapatikana katika Bohari ya Dawa (MSD) na katika mikoa yote kwa ajili ya matumizi ya dharura, hatua inayolenga kuwalinda wahudumu wa afya waliopo mstari wa mbele.

Katika kuimarisha uwezo wa utambuzi wa ugonjwa huo, Serikali pia imesimika maabara mbili jongezi katika mikoa ya Kagera na Kigoma kwa ajili ya kupima sampuli za Ebola karibu na maeneo yanayopakana na nchi zilizoathirika.

Mchengerwa amesema zaidi ya watoa huduma za afya 45,000 wamepatiwa mafunzo ya ana kwa ana na mtandao kuhusu kinga, utambuzi na udhibiti wa Ebola, huku elimu ya afya ikiendelea kutolewa kwa jamii, wasafiri na wananchi wa maeneo ya mipakani.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »