Bodi ya Wakurugenzi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeridhishwa na hatua zinazofanywa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuhakikisha upatikanaji wa Nishati Safi ya kupikia ya Rafiki Briquettes pamoja na kuendeleza kuboresha ubora wa Nishati hii.
Akiongea baada ya ukaguzi wa Kiwanda cha Nishati Safi cha Rafiki Briquettes cha Kisarawe kinachomilikiwa na STAMICO, Mheshimiwa Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu, Mwenyekiti wa Bodi ya REA alisema kuwa bodi imefarijika kuona jinsi
STAMICO walivyopiga hatua ya kujenga viwanda vya kuzalisha Nishati hii ya Rafiki Briquettes ambayo ni mbadala wa matumizi ya Nishati ambazo sio safi kama Kuni na Mkaa.
“Mimi na wenzangu kwenye ziara hii tumefarijika sana kuona jinsi ambavyo wenzetu wa Tumefarijika kuona mfumo mzima wa uandaaji wa Nishati hii na hatua amabazo STAMICO imekuwa ikizichukua kuendelea kuboresha Nishati hii. Kama walivyotuelezea, nishati hii inatokana na vumbi la Makaa ya Mawe (Coal dust) ambayo wanayapitisha kwenye mchakato wa kupunguza hewa za ukaa pamoja na kupunguza ukali wa uwakaji wake” alisema Kingu.
Aliongeza kuwa bodi imefanya utaratibu wa kupata uthibitisho wa Ubora kutoka Shirika la Viwango la Taifa yaani TBS pamoja na kuweka mtambo mdogo wa utafiti ambao unaendelea kufanya tafiti mbali mbali kuhusiana na ubora pamoja na tachnolojia mpya ambapo pia imeridhishwa na jinsi ambavyo wameweka utaratibu mzuri wa kuwafikia wateja ingawa nataka kuona wanaongeza kasi ili kuwafikia Watanzania wengi.
Sambamba na hayo bodi imeridhishwa na kasi ya kuongeza idadi ya Viwanda kufikia vinne ambapo viwili vya Kisarawe na Kiwira vikiwa vinafanya kazi kwa uwezo wa kuzalisha tani 20 kwa saa, kingine cha Tabora kikiwa katika hatua ya uzinduzi na Dodoma katika hatua ya usimikaji wa mitambo.
“Tunajua ajenda kuu ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2034 Watanzania asilimia 80 wanakuwa wanatumia Nishati Safi" alisema Kingu
Katika ziara hiyo Mhe Kingu aliambatana na Mha Hassan Saidy, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mha Sophia Mgonja, Mjumbe wa Bodi, Bwn Stephen Mwakifamba, Mjumbe wa Bodi pamoja na viongozi na watumishi kadhaa kutoka REA.
Lengo kuu la ziara hii ilikuwa kukagua kiwanda cha Rafiki Brequettes Kisarawe kuona shughuli nzima ya uzalishaji na ubora wa bidhaa unavyosimamiwa katika uzalishaji na pia kupata picha ya Kiwanda kipya ambacho REA wametoa ufadhili wa TZS Billioni tatu ambacho kitajengwa Geita.
Naye Mha Hassan Saidy, Mkurugenzi Mkuu wa REA ameitaka STAMICO kuangalia jinsi ya kuwafikia wananchi wengi kwa kuangalia wanavyoweza kushirikiana na Taasisi nyingine za binafsi ili kutekeleza kwa vitendo lengo kuu la kufikisha Nishati hii nchi nzima
Aidha alisema ili kufanikisha adhma ya kuifikisha Nishati Safi nchi nzima STAMICO haina budi kuangalia jinsi ya kushirikiana na taasisi nyingine binafsi ambazo zinaweza kusaidia kusambaza Nishati hii kwa kasi. Aliongeza kuwa REA ipo tayari kutoa ruzuku kwa Taasisi ambazo zinatengeneza majiko banifu ili wananchi wengi waweze kuyanunua na kuweza kutumia Nishati ya Rafiki Briquettes kwa ufanisi.
Katika hatua nyingine tayari REA imekwishatoa ufadhili kwa STAMICO kwa ajili ya kiwanda cha Geita na sasa wapo tayari kutoa ufadhili kwa Kiwanda kingine cha Tanga.
Sambamba na hilo ameongeza kuwa ujenzi wa mitambo ya Kiwanda cha Geita umefika asilimia 50 wakati taratibu za kumpata mkandarasi wa ujenzi wa Kiwanda zikiendelea.
Kwa upande wa Masoko, Mhe Manyama aliwaeleza kwamba tayari taassi kama Magereza zote 129, Kambi za JWTZ,JKT, taasisi za elimu kwa maana ya shule na vyuo, hospitali, masoko ya kuchoma nyama, samaki pamoja na watu binafsi wanatumia Nishati hii ya Rafiki Briquettes.
STAMICO Imejipanga kuendelea kuwa kinara wa kuhakikisha inashiriki kikamilifu katika kuzalisha Nishati hii safi ya Rafiki Briquettes ili kufikia lengo la kufikia asilimia 80 ya matumizi ya Nishati Safi.








EmoticonEmoticon