WCF YAPONGEZWA KWA UTOAJI HUDUMA BORA KWA WANANCHI

December 10, 2025

Na; OWM (KAM) - DODOMA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu amepongeza Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa hatua kubwa ilizochukua katika kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi, hususan wafanyakazi wanaokumbana na madhira ya ajali ama ugonjwa unaotokana na shughuli za kazi.

Pongezi hizo zimetolewa Desemba 10, 2025 Jijini Dodoma alipokutana na Menejimenti ya WCF kwa lengo la kujua majukumu ya mfuko huo sambamba na kutoa maelekezo ya kiutendaji yanayolenga kuongeza tija na ufanisi kuendana na maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Sangu amesema hatua hizo zimechangia kuimarisha imani ya wananchi kwa Mfuko, ambapo wafanyakazi wanaopatwa na madhara kazini wamekuwa wakipatiwa huduma kwa wakati na kwa kiwango kinachostahili, jambo ambalo limeongeza ufanisi na kupunguza usumbufu kwa wafanyakazi waliokuwa na changamoto kazini.

Katika hatua nyingine, Waziri Sangu ameitaka Menejimenti ya WCF kuendeleza ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yao, ikiwemo kubuni mifumo mipya ya kidijitali, kuboresha mbinu za utoaji huduma na kuongeza matumizi ya teknolojia ili kufikia wananchi kwa haraka na kwa ufanisi zaidi.

Awali, akizungumza, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Rahma Kisuo, amehamasisha Menejimenti ya Mfuko huo kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu na huduma zinazotolewa na mfuko, ili kuongeza uelewa na kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Aidha, amesisitiza WCF kuimarisha kampeni za uhamasishaji kupitia majukwaa ya kijamii, vyombo vya habari na mikutano ya wadau ili kuhakikisha taarifa sahihi zinawafikia waajiri, wafanyakazi na jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dkt. John Mduma amesema WCF imejipanga kuendelea kuboresha mifumo ya utoaji huduma ili kuhakikisha madai ya fidia yanashughulikiwa kwa uharaka, uwazi na ufanisi zaidi.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »