UWEKEZAJI MKUBWA ULIOFANYWA NA SERIKALI KITUO CHA GESI ASILIA MLIMANI WALETA NAFUU KWA WANANCHI

December 12, 2025


📌*Kituo kina uwezo wa kujaza gesi asilia kwenye magari na bajaji 800 kwa siku*


📌*Mhe. Salome Makamba ahamasisha Sekta binafsi kuwekeza katika eneo la gesi asilia*


📌*Mikoa ya Morogoro, Dodoma, Arusha, Kilimanjaro na Tanga kufikiwa na vituo vya gesi asilia*


Naibu waziri wa  Nishati Mhe.Salome Makamba ameeleza kuwa, Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika kujenga kituo cha kujaza gesi asilia kwenye vyombo vya usafiri katika eneo la Mlimani jijini Dar es Salaam ambapo zaidi ya sh.Bilioni 12 zimetumika kukamilisha kituo hicho chenye uwezo wa kuhudumia magari madogo na bajaji 800 kwa siku.

Mhe.Salome amebainisha hayo Novemba 12, 2025 Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kukagua kituo hicho kinachosimamiwa na Kampuni Tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania(TPDC) ya GASCO.

 Mhe. Salome ameeleza kuwa Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inahakikisha rasilimali zilizopo zinawanufaisha wananchi kwa namna mbalimbali.

“Matumizi ya gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG) yamerahisisha gharama za maisha kwa watu wa vyombo vya usafiri kwani gharama ya gesi kilo moja ni shilingi 1500 ambapo ukiwa na mtungi wa Kilo 17 unaweza kusafiri umbali wa KM 50 hii inaonesha dhahiri kuwa gesi inagharama nafuu zaidi kuliko mafuta lakini pia kutokana na wingi wa magari ya biashara na bajaji  katika mkoa wa Dar es Salaam uwekezaji huu umekuwa ni fursa kwa wafanyabiashara hao katika kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza kipato.” Amesema Mhe. Salome


Ameeleza kuwa, hadi kufikia Juni 2026 kutakuwa na vituo vingine vya kujaza gesi katika maeneo ya kila  barabara kubwa  ya Mkoa wa Dar es Salaam huku akisiaitiza kuwa Serikali pia imeanza mpango wa kujenga vituo vikubwa katika Mikoa ya Morogoro, Dodoma, Arusha, Kilimanjaro na Tanga ambavyo vitasaidia wananchi wa mikoa hiyo kupata huduma lakini pia wananchi wa Mikoa ya karibu kunufaika na huduma husika.

Mhe.Salome ametoa wito kwa sekta binafsi kuongeza kasi ya uwekezaji katika miundombinu ya gesi asilia, akibainisha kuwa mahitaji ya nishati nafuu yanaongezeka kwa haraka nchini hivyo ni fursa kwao kuwekeza ili kurahisisha upatikanaji wa nishati hiyo kwani Serikali imeboresha mazingira ya uwekezaji kupitia mfumo wa ushirikishwaji wa Biashara kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP) hasa kupitia mfumo wa One Stop Centre ambao ni rahisi kufikisha huduma kwa wananchi. 



Sambamba na hilo amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kutoa kipaumbele kwa vijana kwani sekta ya gesi na mafuta inawagusa moja kwa moja vijana wanaofanya biashara za bolt na bajaji kwani gharama za uendeshaji ni nafuu zaidi.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Bw. Mussa Makame ameeleza kuwa kituo cha kujaza gesi Mlimani  kina uwezo wa kujaza hadi kilogrmu elfu 70 lakini kwa sasa kinajaza hadi kilogramu 50 kwa bajaji, magari madogo pamoja na magari makubwa.


“Zamani kabla ya kujengwa kwa kituo hiki cha Serikali wananchi walikuwa wakijaza gesi katika vituo binafsi ambapo walikuwa wakitumia masaa matatu lakini kwa sasa gari zinatumia dakika nne kujaza gesi na kwa siku kinajaza magari madogo na bajaji 800 lakini magari makubwa 15 yanayopeleka gesi katika vituovidogo.


Amesema  kwa kushirikiana na Sekta binafsi Serikali itahakikisha kufikia 2026 Dar es Salaam inakuwa na vituo vikubwa 15 vya kujaza gesi lakini pia Mikoa ya Pwani, Morogoro, Dodoma, Arusha, Kilimanjaro na Tanga.



Nao wanufaika wa gesi asilia wameishukuru Serikali kwa kuanzisha mradi huo pamoja na  kuendelea kuboresha miundombinu kwani mwanzoni walikuwa wakitumia muda mrefu kujaza gesi lakini kwa sasa wanajaza na kuondoka kwa wakati hali inayowasaidia katika kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza kipato.

#Siku100ZaMhe.RaisNishatiTunatekeleza

#NishatiTupoKazini

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »