PBPA HAKIKISHENI WAWEKEZAJI WAZAWA WANAPEWA KIPAUMBELE KATIKA FURSA ZA UWEKEZAJI -MHE SALOME

December 07, 2025



📌Lengo ni kujenga uchumi wa endelevu unaowanufaisha Watanzania wengi zaidi


📌Aitaka PBPA kuhakisha mafanikio yanayofanywa na Serikali kupitia taasisi  hiyo kujulikana kwa Umma


📍Dar es salaam



Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, ametoa wito kwa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) kuhakikisha wanatoa fursa za uwekezaji kwa wawekezaji wazawa ili kuongeza ushindani na kuimarisha ushiriki wa Watanzania katika sekta ya nishati.


Mhe. Salome ametoa wito huo Novemba 6, 2025 Jijini Dar es Salaam katika ofisi za PBPA, wakati wa ziara yake ya kuzungumza na viongozi wa Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Nishati.

Amesema kuwa ni muhimu PBPA kuweka mazingira rafiki yatakayowezesha makampuni ya ndani kushiriki kikamilifu katika shughuli za uagizaji, usafirishaji na usambazaji wa bidhaa za mafuta.

“ Taarifa kama hii ya uwepo wa   makampuni yanayouza mafuta takribani 86 ambapo makampuni ya nje ni matano tuu inapaswa kujulikana na umma wa watanzania ili dhamira ya serikali ya awamu ya sita  kuwawezesha wazawa ijulikane ili watanzania  kuona wazawa wanapewa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika uwekezaji huu ili tuweze kujenga uchumi endelevu unaowanufaisha Watanzania wengi zaidi,”Amesisitiza Mhe. Salome.

Sambamba na hilo Mhe. Salome ameeleza kuwa ni muhimu kufanya kazi kwa karibu na wafanyabiashara wanaofanya kazi na Taasisi ili kujiimarisha zaidi kiuchumi lakini pia ameelekeza PBPA kuhakikisha wanafanya kazi kwa kushirikiana na Wizara nyingine kwa lengo la kujiimarisha zaidi.

Katika hatua nyingine Mhe. Salome ameeleza kuwa katika kuelezea mafanikio yanayofanywa na taasisi hiyo ni muhimu kazi nzuri inayotekelezwa kuonekana na kueleweka kwa umma kupitia mbinu za kisasa za Mawasiliano huku akisisitiza kuwa katika dunia ya sasa, wananchi wanahitaji taarifa sahihi, za haraka na zinazoeleweka kirahisi ili kutambua thamani ya kazi inayofanywa na serikali pamoja na taasisi zake.

“Niwapongeze kwa kazi nzuri mnayoifanya lakini ili kazi hii ionekane lazima tutumie Mawasiliano ya kisasa ambayo yanafikia watu wengi kwa uwazi na kwa wakati,” amesema Mhe.Salome.


Ameongeza kuwa matumizi sahihi ya  kutoa taarifa zinazofanywa na Taasisi kwa kuwasilisha ujumbe muhimu kwa wananchi zinaweza kuimarisha mahusiano na jamii, kuongeza uwajibikaji na kuhakikisha kila mwananchi anaona matokeo ya kazi inayofanywa kwa manufaa ya Taifa.


Awali akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa kuagiza mafuta kwa pamoja( PBPA) Bw. Erasto Simon ameeleza kuwa   PBPA imeendelea kujiimarisha zaidi katika kuhakikisha mifumo inaboreshwa mara kwa mara lakini pia kuendelea kujifunza kutoka kwa wengine


“Sisi kama PBPA tumeendelea kujiimarisha zaidi katika miundombinu ya mafuta kwani toka tumeanza 2019 mpaka sasa 2025 tumehakikisha nchi inakua na mafuta ya kutosha lakini pia nchi nyingine ikiwemo Zimbabwe Malawi na Msumbiji zimeendelea kuja kujifunza kutoka kwetu hivyo hii ni hatua kubwa zaidi inayoonesha mafanikio katika sekta hii.

Aidha ameeleza kuwa kqtika kuboresha utendaji kazi, Mamlaka ya  Bandari Tanzania (TPA) inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya (Single Receiving Terminal) hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa upokeaji bidhaa za mafuta na kuimarisha ushindani hivyo mradi huu ukikamilika unatarajiwa kupunguza msongamano wa shehena, kuongeza kasi ya huduma na kurahisisha shughuli za kupakia na kupakua mafuta.


#Siku100ZaMhe.RaisNishatiTunatekeleza.

#NishatiTupoKazini.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »