MAADILI KAZINI YAWE MSINGI WA UTOAJI HUDUMA KWA WANANCHI –WAZIRI NDEJEMBI

December 15, 2025



📌*Awataka Watumishi Sekta ya Nishati kujiepusha na rushwa, ubadhirifu na uzembe*


*📌 Asisitiza uzalishaji wa umeme kwa vyanzo mchanganyiko*


*📌 Lengo ni kufikisha megawati 8,000 ifikapo 2030*


*📌 Ataka Elimu ya Nishati Safi ya Kupikia kuwa endelevu*


Watumishi katika Wizara ya Nishati wametakiwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ili kuendelea kutoa huduma bora kwa Watanzania, hususan kwa kujiepusha na vitendo vya rushwa, ubadhirifu na uzembe mahali pa kazi.

 Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratias Ndejembi ameyasema hayo Desemba 15, 2025, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati uliofanyika mkoani Morogoro.

Akizungumza katika mkutano huo, Mhe. Ndejembi amesema  maadili ya kazi ni nguzo muhimu katika kukuza sekta ya nishati na kuharakisha maendeleo ya Taifa, akibainisha kuwa nishati ikiwemo umeme, mafuta na gesi ni mhimili mkubwa wa uchumi wa nchi.

“Zingatieni maadili kazini katika utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kujiepusha na vitendo vya rushwa, ubadhirifu na uzembe mahali pa kazi, ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za umeme, mafuta na gesi,” amesema Mhe. Ndejembi

Aidha, amewataka watumishi wa Wizara kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na weledi ili kuendelea kuchochea maendeleo ya sekta ya nishati na kukuza uchumi wa Taifa.

Kuhusu upatikanaji wa umeme wa uhakika, amesema Wizara ya Nishati ina jukumu la kuhakikisha Tanzania inazalisha jumla ya megawati 8,000 za umeme ifikapo mwaka 2030 kupitia vyanzo mchanganyiko, ikiwemo utekelezaji wa miradi mipya ya uzalishaji umeme.

Ameongeza kuwa katika kufikia lengo hilo, Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itaendelea kuweka vipaumbele sahihi vya nishati  ili kuhakikisha miradi ya kimkakati inatekelezwa kwa wakati.

Vilevile, amewataka watendaji wa Wizara kupitia Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia kuendelea kutoa elimu ya nishati safi ya kupikia  kwa wananchi ili kufikia lengo la asilimia 80 ya Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, kama ilivyoainishwa katika Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema Wizara itaendelea kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya umeme, gesi na mafuta ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma za nishati zilizo bora, salama na za uhakika.




Share this

Related Posts

Previous
Next Post »