Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kushirikiana na Kampuni ya Ukandarasi ya Sinohydro kutoka China inayojenga mradi wa umeme jua Kishapu, limekabidhi miche 10,000 ya miti kwa wananchi wa Kijiji cha Ngunga, Wilaya ya Kishapu, Mkoa wa Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kurejesha bioanuwai ya eneo la utekelezaji wa Mradi wa uzalishaji umeme kwa kutumia Nishati ya Jua wa Kishapu mkoani Shinyanga.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo yaliyofanyika Desemba 18, 2025, Meneja Miradi ya Uzalishaji wa TANESCO, Mhandisi Abdallah Chikoyo, amesema zoezi hilo ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya kijamii na kimazingira ya mradi huo wa kimkakati.
Mhandisi Chikoyo ameeleza kuwa mradi wa umeme wa jua wa Kishapu unatarajia kuzalisha jumla ya megawati 50 za umeme awamu ya kwanza, ambazo zitaimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme katika Mkoa wa Shinyanga na maeneo Jirani ambapo amefafanua kuwa hadi sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia zaidi ya asilimia 84.
“Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, nimekabidhi miche ya miti 10,000 , ambapo miche 9,000 ni ya miti ya kivuli na mbao, na miche 1,000 ni ya miti ya matunda. Lengo ni kuhakikisha kijiji cha Ngunga kinarejea katika hali yake ya awali kimazingira, na tunasisitiza miche hii itunzwe na kulindwa ipasavyo,” alisema Mhandisi Chikoyo.
Kwa upande wake, Afisa Uhusiano wa Kampuni ya Sinohydro aliwashukuru wananchi wa Kijiji cha Ngunga kwa uvumilivu wao wakati wa utekelezaji wa mradi huo, huku akiwahimiza kushiriki kikamilifu katika upandaji na utunzaji wa miti hiyo kwa manufaa ya sasa na ya baadaye ya wananchi na Wilaya ya Kishapu kwa ujumla.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Ngunga, Mussa Mamesa, ameipongeza TANESCO kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika utekelezaji wa zoezi hilo, na kwa niaba ya wananchi wa kijiji hicho, ameahidi kuitunza miche hiyo ili iwe na mchango chanya kwa mazingira kama ilivyokusudiwa.






.jpg)
.jpg)
EmoticonEmoticon