Na Mwandishi wetu- Dar es salaam
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga amewahimiza Watu Wenye Ulemavu kuwa mabalozi wazuri wa kudumisha amani nchini.
Mhe. Nderiananga alieleza hayo wakati wa kikao chake na Wajumbe wa Bodi ya Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) kilichofanyika mwishoni mwa wiki katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu uliopo Magogoni jijini Dar es salaam.
Alisema kwamba, ili shughuli za kiuchumi ziweze kufanyika ni lazima iwepo amani kwani wananchi watakuwa na uhuru wa kufanya shughuli zao bila vurugu zozote hatua itakayochagiza ukuaji wa uchumi wao binafsi hata taifa.
“Tunafahamu yanapotokea madhara watu wa kwanza kuathirika ni watu wenye ulemavu basi tunawashukuru kwa umoja wenu nasi tunawaahidi kuendelea kushirikiana,” alisema Mhe. Nderiananga.
Pia, aliongeza kwamba ipo haja ya Viongozi wa dini kukutana na wakundi ya watu wenye ulemavu kuendelea kuwajenga imani hatua itakayodumisha upendo na mshikamano kama taifa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu katika Ofisi hiyo Dkt. Jim Yonazi alisema, Ofisi hiyo imedhamiria kuwahudumia watu wenye ulemavu pamoja na kusikiliza kero zao ili kuzitafutia ufumbuzi.
![]() |
| U |
“Ofisi ya Waziri Mkuu ni ya utekelezaji wa shughuli za serikali hivyo niwakaribishe katika familia hii naamini tutaendelea kushirikiana na kuhakikisha kila mmoja wetu anafaidika na hadhi ya kuwa mtanzania bila kujali hali yake,”alieleza Dkt. Yonazi.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu (SHIVYAWATA) Bi. Tungi Mwanjala aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna inavyojali watu wenye ulemavu.
Aidha Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Wasiiona (TASODEB) Bw. David Shaba ambaye pia ni mmoja wa wajumbe wa bodi hiyo alishauri watu wenye ulemavu kutokubali kutumiwa na watu wenye nia ovu akisema mahali popote zinapotokea vurugu kundi hilo huathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na kukosa msaada wa haraka.
“Niwaombe wenye ulemavu wenzangu tuwe makini sana tusishawishike hovyo, haya mambo ni ya hatari sana tuzingatie hali zetu hatuwezi kukabiliana na fujo vitakapotokea vita sisi ndio tutaathirika sana zaidi ya hao wanaotuchochea tuwe na msimamo,” alieleza Mwenyekiti huyo.
MWISHOOO





EmoticonEmoticon