Wananchi wa vitongoji vya Chilimba na Mnayope Kata ya Mnyambe Wilaya ya Newala Mkoani Mtwara wamepongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vitongojini chini ya usimamizi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Wametoa pongezi hizo kwa nyakati tofauti Oktoba 20, 2025 wakati wa kampeni maalum ya nyumba kwa nyumba inayoratibiwa na REA ya kuhamasisha wananchi kuunganishiwa umeme na kuutumia kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi.
“Hatukutarajia kama mradi huu wa umeme utatufikia mapema hivi; tunashukuru kwani umeme utasaidia wananchi kuanzisha fursa mbalimbali zinazotokana na uwepo wa umeme kama mashine za kusaga na kukoboa, raia watapata kuamka kimaisha kutokana na kufikiwa na umeme,” alisema Juma Mnandi mkaazi wa Kitongoji cha Chilimba.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mnayope, Sila Kingu alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya kubadilisha maisha ya wananchi wake kupitia nishati ya umeme.
“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais mradi umefika mapema zaidi ya hata tulivyotarajia ni kama historia kwetu maana tulikuwa tunasikia tuu umeme umeme na baadhi ya wananchi hawakuamini kwamba hili linawezekana; lakini kwa uongozi wake umeme umetufikia,” alisema Mwenyekiti Kingu.
Aliipongeza REA kwa kuratibu kampeni hiyo ya nyumba kwa nyumba ambayo alisema kuwa italeta matokeo ya haraka kwani hakuna atakayeachwa nyuma na aliwasihi wataalam katika kampeni hiyo kufanya hivyo kwenye maeneo mengine.
Kingu aliahidi kwa kushirikiana na wananchi watahakikisha miundombinu inatunzwa ili kuendelea kuwanufaisha na kwamba suala la umeme litakuwa ni ajenda ya kudumu kwenye mikutano ya wananchi ili kuendelea kuhamasisha wananchi kuunganishiwa umeme sambamba na kulinda miundombinu.
Naye Stephano Nachilumbwa Mjasiriamali kutoka kitongoji cha Mnayope, anayejihusisha na uuzaji wa vinywaji na mahitaji muhimu ya nyumbani alisema wananchi kitongojini hapo wamekuwa na kiu ya kupata umeme hata hivyo hawakutarajia kuwa ungewafikia katika kipindi cha hivi karibuni.
“Mimi nikiunganisha umeme nitaweka friji hapa ili kuuza vinywaji baridi toifauti na sasa, pia natarajia kumiliki mashine ya kukoboa na kusaga na pia tutahamasishana kama vijana kuona namna bora ya kupata mashine za kubangua korosho maana mimi pia ni mkulima wa korosho,” alisema Nachilumbwa.
Akizungumza katika kampeni hiyo, Msimamizi wa miradi ya REA Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Daniel Mwandupe alisema REA inatumia njia mbalimbali za uhamasishaji ili kuwafikia wananchi kila pande ya nchi ili kutimiza dhamira ya Serikali ya kuleta maendeleo kwa wananchi kupitia umeme.
“Pamoja na mikutano ya hadhara tumefanya kampeni yetu kwa nyumba hadi nyumba ili kuwahamasisha wananchi kuunganishiwa umeme na pia kutumia umeme kujiletea maendeleo vilevile tunatoa elimu ya taratibu za kufuata ili mwananchi aunganishiwe umeme,” alifafanmua Mha. Mwandupe.
Akizungumzia mradi unaotekelezwa Mha. Mwandupe alisema vitongoji vya Chilimba na Mnayope juu vimenufaika na mradi unaotekelezwa na Kampuni ya Sengerema Engineering Group wenye thamani ya shilingi milioni 234 na kwa hatua za mwanzo za mradi kaya zipatazo 81 kutoka katika vitongoji hivyo zitanufaika kwa maana ya wateja wa awali.
“Hizi kaya 81 ni zile ambazo zitaunganishwa katika kipindi hiki ambacho Mkandarasi bado yupo huku na sio kwamba ni hizi tu zitakazounganishwa bali uunganiushaji utaendelea hata pale Mkandarasi atakapoondoka na gharama ni hiyo hiyo ya 27,000 pekee,” alifafanua Mha. Mwandupe.
Alipongeza mwitikio wa wananchi katika vitongoji hivyo ambao alisema wengi wao wamekwisha tandaza nyaya majumbani mwao (wiring) na wanasubiri kuunganishiwa umeme.
“Tumetembelea kaya kadhaa hapa na tumeshuhudia wananchi wapo tayari na wengi wananamatarajio makubwa ya kutumia umeme kujiletea maendele na sio kuwasha taa peke yake,” alibainisha Mha. Mwandupe.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mwandupe, hadi sasa Mkoani Mtwara REA imefikisha umeme katika vitongoji 2,354 kati ya vitongoji 3,421 na kwamba utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme katika vitongoji vilivyosalia mkoani humo unaendelea.
EmoticonEmoticon