REA YAPELEKA NEEMA NANYAMBA

October 28, 2025
-Umeme waibua fursa za kiuchumi

-Wananchi waishukuru Serikali na kuahidi kutunza miundombinu ya umeme

Wananchi wa Kitongoji cha Nyundo; Kijiji cha Nyundo B katika Halmashauri ya Mji wa Nanyamba Mkoani Mtwara wameishukuru na kuipongeza Serikali kwa kuwawezesha kubadili maisha yao kupitia mradi wa umeme uliotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Wametoa shukrani hizo kwa nyakati tofauti kijijini hapo wakati wa Kampeni ya uhamasishaji wa Matumizi ya Umeme kwa ajili ya shughuli za kiuchumi inayotekelezwa na REA katika maeneo mbalimbali Nchini.

"Tunaishukuru Serikali kwa kutufikishia umeme ambao umebadilisha maisha ya wananchi wa hapa; umeme umekuja na fursa nyingi na wananchi hususan vijana wameutumia kuanzisha shughuli mbalimbali za kujiongezea kipato," alipongeza Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyundo B, Hassan Shamte.

Alisema hapo awali wananchi walijishughulisha zaidi na kilimo lakini baada ya kufikishiwa umeme wamebuni miradi mbalimbali inayowaingizia mapato ikiwemo saluni, biashara za vinywaji na shughuli za uchomeleaji yaani welding.

Kwa nyakati tofauti wananchi walipongeza na walifafanua shughuli mbalimbali wanazofanya hivi sasa kwa kutumia umeme ambazo wamesema zimewakwamua kimaisha.

"Umeme umenipa manufaa maana kabla ya umeme changamoto za kimaisha zilikuwa nyingi lakini sasa hivi nina mashine zangu za kunyolea nywele na wateja ni wengi, kazi hii imeniongezea sana kipato," alisema Ramadhan Yusufu Mkazi wa Nyundo.

Naye Hamis Mgulaga fundi uchomeleaji kijijini hapo alisema kupitia umeme ameweza kuendesha maisha yake sambamba na kusaidia wengine katika familia yake kujikwamua kimaisha.

Juma Makoka mkazi wa kitongoji cha Nyundo alisema umeme umefanya awe mtu maarufu kijijini hapo kwa kuanzisha shughuli za kuingiza nyimbo katika simu za wateja wake, kazi ambayo huifanya mida ya mchana baada ya kutoka shamba na nyakati ambazo hakuna shughuli za shamba.

"Umeme unifanya niwe mtu wa kujishughulisha zaidi, hapo kabla nilikuwa nilitoka shamba ni kukaa tuu bila kazi lakini baada ya kufika umeme nikabuni hii kazi na inanisaidia kuendesha maisha," alisema Makoka.

Katika kampeni hiyo ya REA, Wananchi waliohudhuria waliahidi kuwa walinzi wa miundombinu ya umeme na kuwa mabalozi kwa wengine kuhusu kuutumia umeme kujiletea maendeleo

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »