SERIKALI YAWAHAKIKISHIA WAFANYABIASHARA KAWE KUREJEA KAZINI HARAKA

September 16, 2025

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo,akizungumza leo  Septemba 16, 2025, wakati wa ziara yake ya kukagua athari za moto uliotokea alfajiri ya Septemba 15 katika soko la Kawe.

...

SERIKALI  imetenga shilingi milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa soko la muda kwa wafanyabiashara waliokumbwa na janga la moto katika soko la Kawe, huku ikiahidi kukamilisha ujenzi huo ndani ya wiki mbili.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo, ametoa  kauli hiyo leo  Septemba 16, 2025, wakati wa ziara yake ya kukagua athari za moto uliotokea alfajiri ya Septemba 15 katika soko hilo.

Dkt.Jafo amesema kuwa  ujenzi wa soko hilo la muda utafanyika katika viwanja vya Tanganyika Packers, na kumtaka Mhandisi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kuhakikisha kazi hiyo inakamilika kwa muda uliopangwa ili wafanyabiashara waweze kurejea kazini.

“Serikali imejipanga kuhakikisha shughuli za biashara zinaanza tena haraka. Wafanyabiashara wataendelea kutumia soko la muda wakati Serikali ikiendelea na mpango wa kujenga soko la kudumu la kisasa litakalokuwa na miundombinu bora na bima dhidi ya majanga,” amesema  Dkt. Jafo.

Aidha, ametoa  onyo kali dhidi ya kuingilia mchakato wa upangaji wa maeneo katika soko la muda, akisisitiza kuwa ni wafanyabiashara halali pekee ndio watakaopangiwa nafasi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Saad Mtambule, amethibitisha kuwa mbali na shilingi milioni 400 zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa soko la muda, Serikali pia imetenga shilingi milioni 100 kwa ajili ya kuwasaidia wafanyabiashara walioathirika na moto huo.

Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Bi Hanifa Hamza, amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) imedhamiria kujenga soko jipya la kisasa litakalokuwa na mpangilio bora, uzio, na miundombinu ya kisasa ikiwemo bima ya majanga.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »