📌 *Amshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi ya Nishati Jadidifu*
📌 *Afunga mafunzo ya teknolojia ya Nishati ya Jua kwa wataalam*
Tanzania imeendelea kuongeza vyanzo vya kuzalisha umeme kwa kutumia nishati jadidifu hadi kufikia asilimia 67, hii ikijumuisha matumizi ya nishati ya maji na Jua.
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga wakati akifunga mafunzo ya wataalam kutoka taasisi mbalimbali nchini yaliyohusu usanifu, utengenezaji na ufungaji wa mifumo ya Nishati ya Jua pamoja na matumizi yake.
"Tanzania imepiga hatua kubwa katika matumizi ya bora ya nishati na nishati jadidifu ikiwa ni pamoja na Nishati Safi ya kupikia hasa baada ya nchi kutia saini Mpango Mahsusi wa Taifa wa Nishati mwezi Januari mwaka huu, moja ya miradi mikubwa tunayoitekeleza sasa katika nishati jadidifu ni mradi wa umeme jua wa Kishapu mkoani Shinyanga ambao umefikia asilimia 75 na unatarajiwa kuzalisha megawati 50 kwa awamu ya kwanza huku awamu ya pili ikitarajiwa kuzalisha megawati 100." Amesema Luoga
Akifunga mafunzo hayo
Mhandisi Luoga amesema mafunzo kuhusu teknolojia ya nishati ya Jua yamefanyika nchini kwa sababu Tanzania imepiga hatua kubwa katika matumizi bora ya nishati na nishati jadidifu.
Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya Nishati Jadidifu nchini.
Amesema washiriki kutoka katika taasisi mbalimbali wameshiriki mafunzo ya Nishati ya Jua yanayojulikana kama SOLTRAIN + ambayo yameandaliwa na Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Kituo Mahiri cha Matumizi Bora ya Nishati na Nishati Jadidifu (SACREEE) ambacho kipo chini ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi zilizo Kusini mwa Afrika ( SADC).
Awali, mafunzo hayo yalifunguliwa na Mhandisi Felchesmi Mramba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati ambapo aliwataka washiriki hao kutumia ujuzi na maarifa waliyopata katika kujiajiri na pia kutoa ujuzi kwa wengine.
EmoticonEmoticon