WACHIMBAJI WA MADINI SINGIDA WATAKIWA KUWA MFANO WA UADILIFU NA UZALENDO KATIKA UCHIMBAJI

July 18, 2025


_Serikali Yasisitiza Umiliki Halali wa Leseni, Mapato kwa Taifa na Uwekezaji Endelevu_


*Singida, Julai 18, 2025*


Serikali kupitia Tume ya Madini imewataka wachimbaji wa madini ya ujenzi, hususan mchanga, mkoani Singida kuhakikisha wanafanya shughuli zao kwa uadilifu, uaminifu na kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa.


Akizungumza wakati wa kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Singida, Eng. Sabai Nyansiri, amewakumbusha wachimbaji kuwa uchimbaji holela, kutorosha madini au kufanya kazi bila leseni ni kosa la jinai linalozorotesha mapato ya Serikali na maendeleo ya sekta.

“Lazima kila mchimbaji awe na leseni halali  ya madini na apate risiti stahiki wakati wa kufanya malipo. Hii ndiyo njia pekee ya kuhakikisha kuwa michango yao inakwenda serikalini kwa maendeleo ya Taifa,” amesema Eng. Nyansiri.

Amefafanua kuwa leseni za uchimbaji wa mchanga hutolewa kwa kipindi cha mwaka mmoja, na wachimbaji wanapaswa kuzihuisha kwa wakati ili kuepuka kufutiwa au kumpisha muombaji mwingine.


Aidha, Eng. Nyansiri ameeleza kuwa Mkoa wa Singida una fursa nyingi za madini ya ujenzi na unaendelea kushuhudia ongezeko la shughuli za uchimbaji. 

Amesisitiza kuwa Serikali, kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), imejipanga kuendelea kutoa elimu kwa wachimbaji kuhusu uchimbaji salama, endelevu na wenye tija.


_“Tunaendelea kuboresha miundombinu na mazingira rafiki kwa wachimbaji. Vilevile tunakaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya Singida kuja kuwekeza katika madini ya kokoto, mawe na mchanga,”_ ameongeza.

Kwa upande wake, Mjiolojia Geofrey Mutagwa kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Singida, amehimiza wachimbaji hao kujiunga kwenye vikundi au vyama vya ushirika ili waweze kunufaika na fursa za mikopo na huduma mbalimbali za Serikali.

Katika maoni yao, baadhi ya wachimbaji  wa madini waliopatiwa elimu wameeleza kufurahishwa na hatua hiyo ya Serikali. Yusuph Irunde, mchimbaji kutoka mtaa wa Mungumaji, kata ya Kisasida, amesema elimu hiyo imewapa mwanga mkubwa na kuwajengea uwezo wa kuendesha shughuli zao kwa weledi.



_“Tunamshukuru sana Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Singida, Eng. Nyansiri na Serikali kwa kutufikia moja kwa moja. Elimu hii inatuwezesha kuwa wachimbaji bora na wa kisasa’’,_ amesema Irunde kwa furaha.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »