VITONGOJI VYOTE 64,359 VITAKUWA NA UMEME IFIKAPO 2030

July 05, 2025
-Hadi sasa vitongoji 33,657 vimefikishiwa umeme sawa na 52.3%

-Waliofikiwa wasisitizwa kutumia umeme kuibua fursa za kiuchumi

Imeelezwa kuwa hadi kufikia mwaka 2030 vitongoji vyote Tanzania Bara vitakuwa vimefikishiwa nishati ya umeme kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa na kusimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Umeme Vijijini kutoka REA, Mhandisi Jones Olotu Julai 05, 2025 katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) Jijini Dar es Salaam ndani ya Banda la Maonesho la Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

“Tayari tumefikisha umeme katika vijiji vyote 12,318 Tanzania Bara sawa na asilimia 100 na sasa hivi ni zamu ya vitongoji, leo hii ninavyozungumza vitongoji 33,657 kati ya vitongoji 64,359 kote nchini vimefikishiwa umeme ambayo ni sawa na asilimia 52.3,” alisema Mhandisi Olotu.

Mhandisi Olotu aliweka bayana namna ambavyo Serikali imejizatiti katika kuhakikisha umeme unafika katika kila kona ya nchi kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa kwa usimamizi wa REA ili kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Alisema kuwa vitongoji 30,702 havijafikiwa na umeme, hata hivyo alibainisha hatua mbalimbali zilizochukuliwa na zinazoendelea kupitia miradi inayotekelezwa ya kuhakikisha umeme unafika katika vitongoji hivyo.

“Katika vitongoji ambavyo havijafikiwa; vitongoji 7,736 vipo katika miradi inayoendelea kutekelezwa na vitongoji 22,966 kati ya hivi tumetangaza zabuni kubwa ya kufikisha umeme kwenye vitongoji 9,009 hivyo tutabakiwa na vitongoji 13,957 ambavyo tunatarajia ndani ya miaka mitano navyo vitakuwa vimefikiwa kulingana na upatikanaji wa fedha,” alibainisha Mha. Olotu.

Mhandisi Olotu alitoa wito kwa wananchi katika maeneo yaliyofikiwa na umeme kutumia umeme kuboresha hali ya maisha yao kwa kubuni miradi inayotumia umeme ili kujiongezea vipato vyao badala ya kutumia umeme kwa ajili tu ya mwanga wakati wa usiku.

Amewasihi kuiga mfano wa baadhi ya wananchi ambao wamevumbua fursa katika maeneo yao baada ya kufikishiwa umeme jambo ambalo limeanza kuleta manufaa katika maisha yao ya kila siku.

“Baadhi ya wanufaika tumeshuhudia namna ambavyo wamechangamkia uwepo wa umeme kwenye maeneo yao, tumekuta wanatumia umeme kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo saluni, wamefungua kumbi za kuonyesha sinema na mpira, karakana za kuchomelea na wengine wamefungua biashara ya kuuza vinywaji baridi,” alisema.

Alisema kuwa katika maeneo mengi ya vijiji miji hali ya maisha imebadilika baada ya kufikishiwa umeme kwani fursa za ajira zimeongezeka kutokana na kuibuliwa kwa viwanda vidogo vidogo vingi vya kuchakata mazao.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »