TANZANIA YAPOKEA VIFAA VYA MAABARA VYENYE THAMANI YA EURO MILIONI 1.77 KUPITIA MRADI WA QUALITAN WENYE THAMANI YA EURO MILIONI 7

June 19, 2025
Umoja wa Ulaya (EU) umekabidhi rasmi vifaa vya kisasa vya maabara kwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika hafla iliyofanyika katika Makao Makuu ya TBS, Dar es Salaam. 

Hafla hii ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa QUALITAN unaogharimu jumla ya EUR milioni 7, ikiwa ni sehemu ya mradi mpana wa “BEGIN” wenye thamani ya EUR milioni 23 unaolenga kuboresha mazingira ya biashara, kukuza uchumi na kuhimiza ubunifu nchini Tanzania.

Mradi wa QUALITAN unatekelezwa na Shirika la Maendeleo ya Viwanda la Umoja wa Mataifa (UNIDO), ukilenga kuimarisha miundombinu ya kitaifa ya ubora kupitia uboreshaji wa maabara, ujenzi wa uwezo wa taasisi, ubunifu wa kidijitali na kusaidia biashara ndogo na za kati (SMEs).

Kati ya bajeti hiyo, EUR milioni 1.7 zilitengwa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kisasa vya maabara ambavyo sasa vimekabidhiwa rasmi kwa TBS.

Mgeni rasmi wa hafla hiyo,Mkurugenzi wa Maendeleo ya Viwanda kutoa Wizara ya Viwanda na Biashara Bw. Sempeho Nyari, akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo (Mb), alisema “Tunachoshuhudia leo si tu makabidhiano ya vifaa, bali ni alama ya mabadiliko. Mradi wa QUALITAN unalingana kikamilifu na dira ya taifa ya kujenga uchumi wa viwanda unaoshindana kimataifa, unaozingatia mazingira, na unaojikita katika usalama wa bidhaa na ufuataji wa viwango.”

Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi, alieleza mafanikio ya mradi huu, ikiwa ni pamoja na usimikaji wa mashine 38 za kisasa katika maabara za Kemia ya Chakula, Microbiology, Kemia, Umeme na Vipimo (Metrology), Mafunzo ya wafanyakazi zaidi ya 300 wa TBS kuhusu viwango vya kimataifa (ISO/IEC 17025, 17020, 17043).

Balozi wa EU nchini Tanzania, Mhe. Christine Grau, alisema “EU inajivunia kuiunga mkono Tanzania katika kuimarisha miundombinu ya kitaifa ya ubora. Kwa kutoa vifaa hivi kwa TBS, tunaongeza jitihada za Serikali ya Tanzania katika kuboresha ubora wa bidhaa na ushindani wake katika masoko ya kimataifa, ikiwemo soko la EU.”

Mwakilishi wa UNIDO, Bw. Lorence Ansermet, alisifu ushirikiano imara kati ya pande zote na kusisitiza nafasi ya UNIDO katika kulinganisha msaada wa kiufundi na vipaumbele vya maendeleo ya taifa.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TBS, Prof. Othman C. Othman, alisisitiza umuhimu wa sera na utawala bora katika kufanikisha utekelezaji wa mradi.

Bw. Baraka Aligaesha kutoka Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji alisema “Vifaa hivi vitaimarisha uwezo wa TBS kutekeleza majukumu yake ya kimataifa kama vile uthibitishaji, upimaji, na ulinganifu wa viwango, sambamba na kulinda watumiaji, kuongeza mauzo ya nje na kuinua nafasi ya Tanzania katika biashara ya kimataifa, hususan kwa wanawake na vijana.”

Hafla ilihitimishwa kwa wito wa ushirikiano zaidi baina ya taasisi, wadau wa maendeleo na sekta binafsi ili kuhakikisha miundombinu ya ubora nchini inaendelea kuwa nguzo thabiti ya biashara, afya na maendeleo ya kiuchumi.

“Matukio ya leo yawe chachu ya ushirikiano zaidi na uwajibikaji wa pamoja katika kujenga mustakabali ambapo viwango vinaongoza maendeleo na ubora unatawala katika viwanda vyetu,” alihitimisha Bw. Nyari.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »