Mwenyekiti wa Taifa Group na mfanyabiashara mashuhuri, Bw. Rostam Azizi, ametunukiwa Tuzo ya Juu ya Heshima ya Chemba ya Taifa ya Biashara Tanzania (TNCC) kwa kutambua mchango wake katika kukuza uwekezaji, kuunda ajira, kuboresha huduma za jamii na kuchochea maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Tuzo hiyo ilikabidhiwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, aliyekuwa mgeni rasmi katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji la Mwaka 2026 lililoandaliwa na TNCC katika Hoteli ya Johari Rotana, Dar es Salaam.
Akizungumza katika kongamano hilo, Dkt. Mwigulu alisema Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji kupitia maboresho ya sera, sheria, kanuni na mifumo ya utoaji huduma ili kuiwezesha sekta binafsi kuwa injini ya ukuaji wa uchumi na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
"Ajenda ya sekta binafsi ni ajenda ya Taifa. Hatuwezi kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 bila sekta binafsi yenye nguvu na inayoshirikiana kwa karibu na Serikali," amesema.
Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kushughulikia mapendekezo ya sekta binafsi ili kuondoa vikwazo vya biashara na kuongeza ushindani wa bidhaa na huduma za Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Kupitia uwekezaji wake katika sekta mbalimbali, Bw. Rostam Azizi amechangia uundaji wa maelfu ya ajira, kukuza uwekezaji na kuboresha huduma za jamii, hatua zilizochangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Bw. Rostam Azizi aliishukuru Serikali na TNCC kwa kutambua mchango wake, akisema tuzo hiyo ni motisha ya kuendelea kushiriki katika maendeleo ya Taifa."Ninapokea tuzo hii kwa heshima kubwa.
Naihusisha na juhudi za pamoja kati ya sekta binafsi na Serikali katika kujenga uchumi imara. Nawapongeza pia wadau wote waliotunukiwa tuzo mbalimbali leo kwa mchango wao katika kuimarisha sekta binafsi na kukuza uchumi wa Taifa," amesema.
Katika hafla hiyo, Waziri Mkuu pia alikabidhi tuzo mbalimbali kwa wadau wengine, akiwemo Bi. Emma Kawawa, Bw. David Mwaibula, Bw. Imani Kajula, Bw. Elibariki Mmasi na Bi. Mercy Emmanuel Sila, kwa mchango wao katika kuendeleza sekta binafsi, kuboresha mazingira ya biashara na kuimarisha shughuli za TNCC.



EmoticonEmoticon