
Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Hamdouny Mansour (kushoto) akimuonesha muelekeo wa mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Kenya Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Mhandisi Anthony Sanga katika eneo la Holili mjini wilayani Rombo alipotembelea eneo hilo Juni 23, 2025.
……..
Na Munir Shemweta, WANMM ROMBO
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga ameoneshwa kuridhishwa na kazi ya uimarishaji mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Kenya.
“Nimefurahi na kuridhishwa kwa kazi iliyofanyika ya kuimarisha mpaka wetu na nduguzetu wa kenya na niseme ni mfano mzuri wa kazi ya uimarishaji mpaka kwa nchi tunazopakana nazo” amesema.
Mhandisi Sanga ameridhishwa na kazi hiyo alipotembelea kijiji cha Usongo na Holili Mjini wilayani Rombo mkoa wa Kilimanjaro tarehe 23 Juni 2025 kuangalia maendeleo ya zoezi la uimarishaji mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Kenya.
Kwa mujibu wa katibu mkuu wa wizara ya Ardhi, kati ya kilomita 758 za mpaka wa kimataifa kati ya nchi hiźo mbili tayari kilomita 558 zimeimarishwa na kueleza kuwa hilo ni jambo zuri na la kujipongeza.
“Kwa kweli niseme tu kuwa, ile timu iliyokuwa uwandani imenifurahisha na tutaona cha kufanya katika sehemu ya kuwashukuru zaidi” ameeleza.
Ameongeza kwa kusema, utaratibu wa kusainiwa Hati ya Makubaliano (MoU) kama ilivyotumika wakati wa kuimarisha mpaka wa Tanzania na Kenya utumike pia katika mipaka mingine ili kuongeza kasi ya uimarishaji mipaka ya kimataifa.
Kwa upande wake Mratibu wa zoezi la uimarishaji mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Kenya Bw. Robert Paul ameeleza kuwa, katika awamu ya nne na tano ya uimarishaji mpaka wa nchi hizo,Tanzania imetekeleza kazi zake zote kwa wastani wa asilimia 95.
” Kwa upande wetu kazi ya ujenzi tumetekeleza kwa asilimia 100, kazi ya kufyeka kama asilimia 95, mkuza imekamilika asilimia 91 hivyo wastani wa asilimia 95 ya kazi zote imeamilika” amesema.
Mpaka wa Tanzania na Kenya upande wa eneo la nchi kavu una ukubwa wa Kilomita 758 na uimarishaji wake mbali na mambo mengine utasaidia kuondoa baadhi ya changamoto zilizokuwa zikijotokeza kwa wananchi wanaofanya shughuli katika maeneo ya mipakani.
Zoezi la uimarishaji mipaka ya kimataifa ni utekelezaji wa makubaliano ya Umoja wa Afrika kuwa, ifikapo mwaka 2027 mipaka baina ya nchi za Afrika iwe imeimarishwa.
Tanzania imepakana na nchi 10 ambazo ni Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zambia, Malawi, Msumbiji, Comoro na Shelisheli huku mipaka baina ya nchi hizo ikiwa imegawanyika katika sehemu mbili za nchi kavu na majini.

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga (wa pili kulia) akiangalia moja ya alama za mpaka wa kimataifa kata ya Tanzania na Kenya katika kijiji cha Usongo wilayani Rombo mkoa wa Kilimanjaro alipotembelea eneo hilo Juni 23, 2025. Kulia ni Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi Hamdouny Mansour.

Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Hamdouny Mansour (kushoto) akimuonesha muelekeo wa mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Kenya Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Mhandisi Anthony Sanga katika eneo la Horiri mjini wilayani Rombo alipotembelea eneo hilo Juni 23, 2025.

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga (kulia) akieleza jambo kwa watendaji wa Wizara yake alioambatana nao alipotembelea mpaka wa kimataifa kata ya Tanzania na Kenya katika eneo la Horiri Mjini wilayani Rombo mkoa wa Kilimanjaro Juni 23, 2025. Wa tatu kushoto ni Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi Hamdouny Mansour.(PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
EmoticonEmoticon