📌 Asema ni Nishati yenye unafuu wa gharama kulinganisha na vyanzo vingine vya nishati, pia isiyochafuzi kwa mazingira.
📌 Asisitiza nyuklia kwa ajili ya kuzalisha umeme ni salama, awatoa hofu jamii kuhusiana na matumizi yake
📌 Akazia kuhusiana na matumizi ya Vinu vidogo vinavyotumia teknolojia ya kisasa ya Small Module na Micro Reactors
📌 Nyuklia yatajwa kuleta mapinduzi ya kweli ya uchumi na viwanda Afrika
📌 Rais Samia adhamiria Tanzania kuzalisha umeme wa nyuklia
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Tanzania inatarajia kuzalisha umeme unaotokana na nyuklia utakaojumuishwa katika Gridi ya Taifa ili kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya umeme yanayotokana na ongezeko la viwanda.
![]() |
Dkt. Biteko amesema hayo Juni 30, 2025 Kigali nchini Rwanda wakati akihutubia katika Mkutano kuhusu masuala ya Nyuklia Afrika.
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeiagiza Wizara ya Nishati chini ya uongozi wangu kuhakikisha kwamba hivi karibuni umeme utakayozalishwa unajumuishwa katika Gridi ya Taifa,” amesema Dkt. Biteko.
![]() |
Ameongeza kuwa kupitia agizo hilo Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali ikiwemo kuandaa mikakati ya pamoja ya taasisi za Serikali ili kufikia azma ya kuzalisha umeme wa nyuklia kwa kuwa ni nishati yenye unafuu wa gharama kulinganisha na vyanzo vingine vya nishati, pia isiyochafuzi kwa mazingira.
Ametaja baadhi ya jitihada kuwa Juni 2025 Tanzania iliandaa warsha ili kutoa uelewa kwa wadau wa masuala ya nyuklia ikiwa ni pamoja na kuanzisha taasisi itakayoratibu na kusimamia shughuli za nyuklia.
“Serikali yangu itahakikisha inaendeleza mazingira mazuri kwa ajili ya uzalishaji wa nishati kwa kutumia nyuklia kwa kutunga sera thabiti na kuanzisha mifumo ya sheria na udhibiti kwa ajili ya usimamizi wa raslimali ya nyuklia na uzalishaji wa umeme unaotokana na nyuklia, amesisitiza Dkt. Biteko.
Vilevile amesema Serikali itaongeza raslimali watu wenye ujuzi katika teknolojia za nyuklia ili kutumia kikamilifu raslimali hiyo hususan katika maeneo mengine ikiwemo afya na kilimo.
Amesema tayari Tanzania ina nyaraka mbalimbali zinazoiangazia nyuklia kama raslimali ya msingi kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya nishati ya baadae kama vile Sera ya Taifa ya Nishati, Mkakati wa Nishati Jadidifu na Sera ya Maendeleo ya Madini.
Hata hivyo amesema Serikali ina lengo la kuimarisha Sera ya Teknolojia ya Nyuklia ya mwaka 2013 ili kiakisi maendeleo ya hivi karibuni sambamba na kufuata viwango vya kimataifa.
Akifungua Mkutano huo Waziri Mkuu wa Rwanda Mhe. Dkt. Edward Ngirente amesema kuwa ili kufikia Mpango wa Maendeleo wa Rwanda wa mwaka 2050 wa kuwa nchi ya kipato cha juu wanahitaji kuwa na uzalishaji wa umeme kwa kiasi kikubwa.
“ Hivyo, Rwanda tumeamua kuzalisha umeme wa nyuklia kwa kuwa ni salama na wa uhakika na hauhitaji mvua ili kurahisisha maendeleo kwa kutumia teknolojia,” amesema Mhe. Ngirente.
Aidha, amesema Mkutano huo wa nyuklia utakuwa na manufaa kwa Afrika katika kusaidia maendeleo. Pia nchi za Afrika kwa pamoja lazima ziwe kinara katika matumizi ya nishati safi na kuwa muda wa utekelezaji ni sasa ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira na ongezeko la idadi ya watu.
Waziri Mkuu wa Niger, Mhe. Ali Mahamane Lamine Zeine amesema kuwa nchi yake ina vyanzo vingi vya nishati ikiwemo maji na sasa imezindua mpango wake wa nyuklia hivyo nyuklia ni nishati safi na ina manufaa makubwa katika uzalishaji wa umeme barani Afrika.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Mionzi ya Atomiki Rwanda, Dkt. Lassina Zerbo amesema kuwa Rwanda ipo katika hatua za mwishoni za kuanzisha vinu vya nyuklia vya kuzalisha umeme.
Ameongeza kuwa katika kufikia hatua hiyo ilihitaji dhamira ya viongozi na imani kwa wananchi juu ya umuhimu wa uzalishaji wa umeme wa nyuklia.
Mkutano huo unaofanyika kuanza Juni 30 hadi Julai 1, 2025 nchini humo unajumuisha wadau wa nishati kutoka ndani na nje ya Afrika wenye lengo la kuharakisha matumizi ya nyuklia kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kuleta mabadiliko ya nishati Afrika.
Mwisho
EmoticonEmoticon