MWANA FA AMHAKIKISHIA MCC RAJAB USHINDI WA CCM ASILIMIA 100 KATA YA NKUMBA

October 24, 2025

 



**πŸ“ Mgombea Ubunge Aahidi Kushughulikia Uzio wa Sekondari kwa Fedha za Mfukoni Ikiwa Serikali Itachelewa**


**πŸ“ Ustadh Rajab Asema CCM Ni Mwalimu wa Siasa, Awataka Wananchi Walinde Amani**


**Na Mwandishi Wetu, Kata ya Nkumba**


MGOMBEA Ubunge Jimbo la Muheza kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), **Hamis Mwinjuma**, maarufu kama **MwanaFA**, amemhakikishia Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM (MCC), **Ustadh Rajab Abdulrahaman Abdallah**, kwamba chama hicho kitashinda Kata ya Nkumba kwa asilimia 100.


Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika Kijiji cha Nkumba-Kisiwani, MwanaFA alisema ushindi huo unatokana na idadi kubwa ya wanachama wa CCM waliojiandikisha katika kata hiyo.


Alifafanua kuwa katika kata hiyo, idadi ya wanachama wa CCM ni **4,984**, huku idadi ya watu waliojiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ikiwa ni **4,807**.

"Ndugu Mwenyekiti, ukitazama wanachama wetu na watu waliojiandikisha, unaona kabisa tunakwenda kushinda. Nikutoe hofu, hapa tutashinda kwa asilimia 100 kura za Rais, mbunge na diwani, kama tu hatutakuwa tumekwanza wenyewe kwa wenyewe," alisema MwanaFA.


### **Sifa kwa Rais Samia na Miradi Iliyotekelezwa**


Mgombea huyo aliwaomba wananchi wa Nkumba kuhakikisha wanajitokeza kupiga kura na kuwachagua wagombea wa CCM.


Alisisitiza kuwa anasimama kifua mbele kumuombea kura **Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan** kutokana na kazi kubwa aliyoifanya Nkumba. Alibainisha kuwa ndani ya miaka minne na nusu, Rais Samia ameleta jumla ya **Shilingi Bilioni 2.1** kutekeleza miradi mbalimbali:


* **Elimu:** Sh. Milioni 121.9 zilitolewa kwa ajili ya Sekondari ya Nkumba, na Sh. Milioni 115.5 kwa Elimu ya Msingi kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, na ukarabati.

* **Afya:** Sh. Milioni 49.3 zilitumika kwa ajili ya ujenzi wa zahanati.

* **Maji:** Mradi wa Sh. Milioni 630 uliwezesha uchimbaji wa visima vinane, ambapo kila kitongoji katika vijiji vitano vya kata hiyo kilipata kisima kimoja.

* **Umeme:** Sh. Milioni 345 zimetumika kufikisha Umeme katika vitongoji na vijiji.

* **Huduma za Jamii:** Vikundi vitano vya wajasiriamali vilipata Sh. Milioni 34, na vijiji vyote vimenufaika na TASAF.

### **Ahadi za Miaka Mitano Ijayo**


MwanaFA, ambaye mkutano huo ulikuwa wa mwisho katika kata zote 37 za jimbo lake, aliahidi mambo makuu atakayotekeleza katika miaka mitano ijayo:


1.  **Ujenzi wa Uzio (Fensi):** Ujenzi wa uzio wa Sekondari ya Nkumba, akiahidi kutoa **fedha zake za mfukoni** iwapo Serikali itachelewa kuleta fedha.

2.  **Kipaumbele:** Kushughulikia na kukamilisha miradi yote iliyoanzishwa na serikali katika sekta za Elimu, Afya, Maji, Barabara, na Umeme.

3.  **Maji:** Kuchimba visima katika vijiji vya **Kwemhosi** na **Ubembe**.

### **Ustadh Rajab Atoa Onyo Kuhusu Amani**


Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, **Ustadh Rajab Abdulrahaman Abdallah**, aliwaongoza vijana na wazee kukumbuka historia ya Tanzania tangu ilipoasisiwa.

Alisisitiza kuwa **CCM ni Mwalimu wa vyama vya ukombozi** Kusini mwa Jangwa la Sahara na ndio maana inashinda kila uchaguzi, kutokana na misingi miwili mikuu: **Kutekeleza Ilani yake** na **Kulinda Amani**.


Ustadh Rajab aliwataka wananchi wasiharibu amani iliyopo kwa kisingizio cha uchaguzi, akionya kuwa Tanzania ndiyo nchi pekee ya kukimbilia katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.

"Tusifanye utani hata kidogo na amani hii. Twendeni tukachague wagombea wa CCM ili wawaletee maendeleo pamoja na kulinda Amani. Wenzetu wakiuana huko hawana pa kukimbilia isipokuwa nchini kwetu. **Kuchagua CCM ni kuchagua Amani**," alisema, akitaja Burundi, Rwanda, na Msumbiji kama nchi zilizowahi kuhifadhi wakimbizi Tanzania.

### **Viongozi Wengine Wamtia Nguvu MwanaFA**


Naye mgombea Udiwani wa Kata hiyo, **Omar Kidundai**, aliahidi kushirikiana na mbunge na Rais kutatua changamoto zote. Alisema ametumia mikutano 18 kuomba kura na wananchi wameahidi kuwachagua wagombea wa CCM.

Kwa upande wake, **Balozi Adadi Rajab**, aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Muheza (2015-2020), alimtaja MwanaFA kama mbunge mwenye uwezo wa kusukuma maendeleo na anatosha kuendelea kuaminiwa.

"Mimi kule bungeni nilipokuwa nilikuwa naongea sana, lakini niliambulia kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama. Lakini MwanaFA alipoingia kule, ametufanyia kazi nzuri na Rais amempa Uwaziri. Nasema mbele yenu **sitagombea tena ubunge Muheza, MwanaFA anatosha**," alisema Balozi Rajab.


Mratibu wa Kampeni Jimbo la Muheza, **Swahibu Mwanyoka**, aliwataka wananchi kuachana na wagombea wa upinzani kwa kuwa hawana nia ya kuwaletea maendeleo, na akawaonya wasiwe na hofu kwani vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga.



Share this

Related Posts

Previous
Next Post »