Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Ireland anayeshughulikia ushirikiano wa kimataifa, maendeleo, na diaspora, Mhe. Neale Richmond, amefanya ziara rasmi mkoani Tanga kwa lengo la kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayofadhiliwa na Serikali ya Ireland.
Katika ziara yake, Mhe. Richmond alitembelea Mradi wa Faida Maziwa, unaotekelezwa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI). Mradi huo unalenga kuboresha uzalishaji wa maziwa, kuongeza thamani ya bidhaa za maziwa, na kuinua kipato cha wafugaji wa ng’ombe wa maziwa.
Aidha, ameweka mkazo katika matumizi ya mbegu bora za malisho, hatua inayosaidia kupunguza migogoro kati ya wafugaji na wakulima, na hivyo kuimarisha ustawi wa maisha ya jamii ya wakulima na wafugaji mkoani Tanga.
Pia, Mhe. Richmond alitembelea kituo cha afya kinachofadhiliwa na Benjamin Mkapa Foundation kwa kushirikiana na Shirika la Afya la Amref, ambacho ni miongoni mwa taasisi zinazopokea msaada kutoka Serikali ya Ireland.
Katika ziara hiyo, alishuhudia juhudi zinazofanywa katika kuboresha huduma za afya, hususan afya ya mama na mtoto, pamoja na uwekezaji katika miundombinu ya huduma za afya.
Aidha, Waziri Richmond alipata fursa ya kuzungumza na viongozi wa mashirika mbalimbali yakiwemo Amref, Benjamin Mkapa Foundation, Femina, na Uzikwasa, pamoja na vikundi vya kijamii vinavyotekeleza miradi ya maendeleo katika sekta tofauti.
Akihitimisha ziara yake mkoani humo Mhe. Richmond alisisitiza dhamira ya Serikali ya Ireland kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza maendeleo endelevu kupitia miradi yenye tija kwa wananchi.
Pia alitoa pongezi kwa wadau wote wanaoshiriki katika utekelezaji wa miradi hiyo na kusisitiza kuwa ni muhimu kuimarisha sekta za afya, kilimo, na biashara ili kukuza uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.
EmoticonEmoticon