Morogoro – Tanzania imepiga hatua muhimu katika sekta ya misitu baada ya wataalamu wa misitu kutoka Russia kutembelea Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) kwa lengo la kujadili na kuimarisha utafiti wa kisayansi katika uhifadhi wa misitu.
Ziara hiyo iliyofanyika Machi 11,2025, iliyojumuisha maofisa wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wakiongozwa na Kamishna wa Uhifadhi, Profesa Dos Santos Silayo, ililenga kuboresha ushirikiano wa kisayansi, kielimu na kiteknolojia kati ya Tanzania na Russia katika sekta ya misitu na uhifadhi wa mazingira.
Wataalamu hao wa misitu, wakiongozwa na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Ufundi wa Misitu cha Jimbo la Saint Petersburg, Chuo Kikuu cha Petrozavodsk na Chuo Kikuu cha Misitu na Teknolojia cha Jimbo la Voronezh, walijadili maeneo mbalimbali ya utafiti wa pamoja. TAFORI iliwasilisha tafiti muhimu zilizoainisha fursa za kushirikiana katika nyanja za ikolojia, usimamizi wa misitu na teknolojia za kisasa za uhifadhi wa mazingira.
Akizungumza katika kikao hicho, Profesa Silayo alieleza kuwa ushirikiano huu unalenga kutatua changamoto zinazokabili sekta ya misitu, ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, magonjwa ya mimea na matumizi ya teknolojia bunifu kama setilaiti na ndege zisizo na rubani (drones) katika usimamizi wa misitu.
“Ushirikiano huu unaleta pamoja wataalamu wa Tanzania na Russia, na tunatarajia kunufaika kupitia kubadilishana maarifa na uzoefu wa kisayansi,” alisema Profesa Silayo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAFORI, Dk Revocatus Mushumbusi, alisisitiza umuhimu wa kushirikiana katika utafiti wa misitu, hususan katika kukabiliana na moto wa misitu na kuendeleza mbinu za kisasa za utafiti.
“Ushirikiano huu utatufundisha mbinu mpya na teknolojia zinazotumika Russia, ambazo zinaweza kusaidia kuboresha uhifadhi wetu wa misitu,” alisema Dk Mushumbusi.
Watafiti kutoka Russia walielezea mafanikio yao katika matumizi ya teknolojia za kisasa kama setilaiti na drones ili kutathmini hali ya misitu kwa ufanisi mkubwa. Aidha, waligusia umuhimu wa utafiti wa pamoja katika maeneo ya uzalishaji wa miti bora, entomolojia na matumizi ya teknolojia ya akili mnemba (AI) katika usimamizi wa misitu.
Mtafiti Mkuu wa TAFORI, Dk Chelestino Peter Balama, alibainisha kuwa taasisi hiyo imepiga hatua katika uhifadhi wa mazingira na kulinda mimea iliyo hatarini kutoweka, akisisitiza kuwa ushirikiano huu utaongeza ufanisi katika juhudi hizo.
Ziara hii inatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo zaidi katika sekta ya misitu kwa kubadilishana ujuzi, utafiti na teknolojia kati ya Tanzania na Russia, ikiwa ni hatua muhimu katika kuhakikisha uhifadhi endelevu wa misitu nchini.
Tulizo Henry Kilaga I A Brand Communication Strategist,
EmoticonEmoticon