DC MWANGA WANAWAKE WANAPASWA KUJIAMINI NA KUITUMIKIA JAMII KWA HAKI

March 01, 2025

 


 Na Ashrack Miraji Tanga Raha

Mwanga, Kilimanjaro – Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Mhe. Mwanahamis Munkunda, amewataka wanawake, hususan vijana, kutumia nafasi wanazozipata kwenye taasisi mbalimbali kwa kujituma na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Akizungumza katika maandalizi ya Siku ya Wanawake Duniani, ambayo kitaifa itafanyika mkoani Arusha, Mhe. Mwanahamisi aliwahimiza wanawake kuwa na umakini katika kazi zao, akisisitiza kuwa ni muhimu kuzingatia haki na kutimiza majukumu yao kwa ufanisi.

"Ninachotaka kusema katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, wale tunaopata nafasi basi  tuzitendee haki hasa tunapotoa huduma kwa wananchi," alisema Mhe. Mwanahamis akizungumza mbele ya wakazi wa wilaya hiyo.

Pia, alizungumzia mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika harakati za kutetea haki za wanawake, akisema kuwa tofauti na miaka ya nyuma, sasa haki za wanawake zinatambuliwa na kuheshimiwa, jambo linaloongeza motisha kwa wanawake wengi kushiriki katika uongozi na shughuli za maendeleo.

"Miaka ya nyuma hakukuwa na haki kwa wanawake katika masuala mbalimbali, lakini sasa haki zao zinatambuliwa na kuheshimiwa," aliongeza Mhe. Mwanahamis 

Aidha, alisisitiza kuwa usawa unapaswa kuonekana kati ya wanawake na wanaume katika jamii, na kupongeza Serikali ya Tanzania kwa juhudi zake katika kuhakikisha utekelezaji wa usawa katika utekelezaji wa majukumu.

Akitoa mfano wa utekelezaji wa usawa, Mhe. Mwanahamis alimtaja Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kama mfano bora wa uongozi wa kike na kuhimiza wanawake kujiamini na kushika nafasi mbalimbali za uongozi.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »