HAPI AZIFUMUA HOJA ZA TUNDU LISSU NA CHADEMA KUHUSU "UCHAGUZI MKUU"

February 23, 2025



Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Ally Hapi, amesema kauli za Mwenyekiti wa Chadema na viongozi wengine wa Chama hicho kuhusu kuzuiya uchaguzi mkuu hazina hoja wala mashiko, bali ni dalili za kuwa Chama hicho hakijajiandaa na uchaguzi Mkuu ujao.


Hapi ameyasema hayo wakati akizungumza na wanachama wa CCM na Jumuiya ya Wazazi wilayani Muheza, mkoani Tanga ikiwa ni sehemu ya mapokezi ya Rais Samia Suluhu Hassan mkoani Tanga kwa ziara ya kikazi.


Akichambua hoja moja baada ya nyingine, Hapi amesema kauli hizo zinakinzana na ukweli kwamba yako mabadiliko yaliyofanyika katika sheria za uchaguzi nchini mwaka 2024, ambayo pamoja na mambo mengine yameondoa kupita bila kupingwa, kuundwa Tume huru ya uchaguzi (INEC) na kuondoa ulazima wa Wakurugenzi kuwa wasimamizi wa uchaguzi na badala yake sheria kutamka kuwa afisa mwandamizi wa serikali atateuliwa na tume kuwa msimamizi wa uchaguzi.


Hapi amebainisha kuwa, katika mchakato wa mabadiliko hayo ya sheria za uchaguzi mwaka 2024, wadau wote walishirikishwa na kutoa maoni ikiwemo CHADEMA, taasisi za dini, taasisi za kiraia, vyama vingine vya siasa na wananchi kwa ujumla.


“CHADEMA walitoa maoni yao kama wadau, na baadhi ya maoni hayo yaliingia katika sheria. Kama wanabisha kuwa hawakushiriki kutoa maoni watoke hadharani wakatae.” Alisema Hapi.


Kuhusu hoja ya Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu ya kutaka uchaguzi mkuu usogezwe mbele, Hapi ameeleza kuwa huko ni kuwanyima haki wananchi ya kuchagua viongozi wao na kwamba kuna kila sababu ya kuamini kuwa CHADEMA kama Chama haijajiandaa kwa uchaguzi, na kwamba wanatafuta visingizio kutaka uchaguzi mkuu usogezwe mbele kinyume cha sheria ili wapate kutafuta fedha kwa wafadhili wao na kuponya majeraha ya ndani ya Chama chao yaliyotokana na uchaguzi wa ndani.


“Wenzetu hawajajiandaa kwa uchaguzi. Wako dhaifu na wana ukata mkubwa, ndiyo maana katika uchaguzi wa serikali za mitaa yako maeneo mengi walishindwa kusimamisha wagombea. ” Amesema Hapi.


Katika hatua nyingine, Hapi amevitaka vyombo vya dola kufanyia kazi kauli zenye lengo la kubagaza sheria za nchi na kuvuruga amani ikiwemo kauli ya kutaka kuzuiya uchaguzi mkuu ambao uko kwa mujibu wa sheria.


Hapi amewataka wananchi wawapuuze wanaotaka kuvuruga amani ya nchi na kwamba uchaguzi mkuu utafanyika kama ilivyopangwa na CCM itashiriki uchaguzi huo.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »