TANZANIA YAJIVUNIA USHIRIKIANO KATI YAKE NA KUWAIT

February 20, 2025


Na Happiness Shayo-Dar es Salaam


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inajivunia ushirikiano wa kidiplomasia uliopo kati yake na nchi ya Kuwait katika biashara, uchumi na kwa kuwa na  uongozi bora.


Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) ameyasema hayo leo Februari 20, 2025 katika Maadhimisho ya Miaka 64 ya Uhuru na Maadhimisho ya Miaka 34 ya Ukombozi wa Jimbo la Kuwait yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

“Wakati Kuwait inaadhimisha tukio hili muhimu leo nina furaha kuwafahamisha kuwa uhusiano wetu wa nchi hizi mbili unazidi kuwa bora na kuna juhudi za kuimarisha zaidi uhusiano huu wa kirafiki zinaendelea, chini ya uongozi mahiri wa viongozi wetu wawili, Amir wa Kuwait ,Mtukufu Sheikh Mishal al-Ahmad al-Sabah na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan” amesema Mhe. Chana.

Amefafanua kuwa kupitia ushirikiano huo baadhi ya bidhaa za Tanzania zinapatikana katika maduka makubwa ya Kuwait ikiwa ni pamoja na nyama, matunda na mbogamboga.


Mhe. Chana ametumia fursa hiyo kualika Ubalozi wa Kuwait nchini Tanzania kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa lengo la kuongeza watalii kutoka nchini Kuwait na kuvinadi vivutio vya utalii vilivyoko nchini Tanzania ikiwemo uzuri wake wa asili na utajiri wa utamaduni, kutoa uzoefu wa kipekee na usioweza kusahaulika.

Katika hatua nyingine, Mhe. Chana ameweka bayana kuwa Kuwait imekuwa ikiisaidia Tanzania katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo mradi wa Maji Same-Mwanga, mradi wa Umwagiliaji wa Bonde la Mto Luiche, barabara ya Nyahua - Chaya na maendeleo mengine ya miundombinu.

“Utiaji saini wa Makubaliano ya ushirikiano kati ya Taasisi zetu mbili za Kidiplomasia, Kituo cha Mahusiano ya Kigeni cha Dk. Salim Ahmed Salim na Taasisi ya Diplomasia ya Saud Nasser Kuwait mwezi Desemba mwaka jana 2024 ni hatua muhimu katika uhusiano wetu baina ya nchi hizo mbili, hii itahakikisha wanadiplomasia kutoka nchi zetu wana ujuzi na maarifa ya kutekeleza majukumu yao kwa weledi hivyo kuwa nguzo muhimu katika ushirikishwaji wetu wa masuala ya kimataifa” amesema Mhe. Chana.

Naye, Balozi Mdogo,  Ubalozi wa Kuwait,  Musad Ali  Aldhubaib amesema kuwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Kuwait na Tanzania umeendelea kukua kwa kasi  tangu mwaka 2015 ambapo nchi hizo mbili zilifungua  balozi baina yao.





Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi (Mb), Balozi wa Muungano wa Comoro na Mkuu wa Kikosi cha Wanadiplomasia, Mhe. Ahamada- El Badaoui Mohamed, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, Mhe. Balozi Abdalah Kilima, Waheshimiwa Mabalozi, Makamishna Wakuu, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na Viongozi Waandamizi wa Serikali.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »