RAIS DKT SAMIA KUPOKEA TUZO YA "THE GATES GOALKEEPERS AWARD

February 03, 2025


Na WAF - Dar Es Salaam

 

Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajia kupokea tuzo ya “The Gates Goalkeepers Award” kama kielelezo cha matokeo makubwa ambayo yamepatikana kwenye uongozi wake kufuatia ripoti ya utafiti wa demografia na afya ya mwaka 2022 inayoonesha kupungua kwa vifo vitokanavyo na uzazi kwa asilimia 80.

 

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo  Februari 3, 2025 wakati akitoa taarifa ya upokeaji wa tuzo hiyo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zinazoandaliwa na taasisi ya The Gates Foundation, mbele ya waandishi wa habari kwenye ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.


Waziri Mhagama amesema tukio hilo linafanyika nje ya Marekani nchini ya Tanzania kwa mara ya kwanza na Rais Samia ndiye kiongozi wa kwanza kupokea tuzo hiyo kwa bara la Afrika jambo lililochochewa na uongozi wake mahiri ulioleta mafanikio makubwa nchini hususani ni sekta ya afya kwa kuitendea haki na kusababisha mataifa makubwa duniani kutambua mchango wake.

 

Amesema kuwa mafanikio haya yametokana na mikakati mbalimbali iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa kutokana na utashi wa kisiasa chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia kuweka mazingira wezeshi kisera pamoja na  kuimarisha rufaa za akina mama na watoto. 

 

“Rais Samia ameongeza bajeti ya kuimarisha huduma ikiwemo upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, kusogeza huduma za dharula za uzazi karibu na wananchi kwa kujenga zaidi ya vituo 530 vya upasuaji wa kutoa mtoto tumboni,” amesema Waziri Mhagama

 

Waziri Mhagama ameipongeza Taasisi ya The Gates Foundation kwa kutambua na kuunga mkono juhudi za serikali kwenye kupambana na vifo vitokanavyo na uzazi, Watoto wachanga na walio na umri chini ya miaka mitano (5).

 


“Kwa namna ya kipekee, tunatambua jitihada za kipekee za Amiri jeshi Mkuu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mapambano ya vifo vya kina mama vinavyotokana na uzazi, vifo vya Watoto wachanga na Watoto walio chini ya miaka mitano, hivyo wananchi wenzangu tunayo kila sababu ya kumpongeza na kutembea kifua mbele kwa jinsi Mheshimiwa Rais anavyotung’arisha nchi yetu nje ya mipaka ya nchi yetu,” amesema Waziri Mhagama

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »