Mfumo wa kidijitali wa JKCI kuboresha usajili na matibabu ya wagonjwa

July 16, 2026
Na Mwandishi Wetu, Arusha

Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), imezindua mfumo wa kidijitali wa usajili wa wagonjwa na teknolojia mpya ya kisasa ya Dozee ya kufuatilia hali ya mgonjwa hata kiwa nyumbani.

Uzinduzi huo ulifanyika jana jijini Arushwa ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini,Paul Makonda.

Alisema uwekezaji huo unaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoendelea kupiga hatua barani Afrika katika matumizi ya ubunifu wa kidijitali kuboresha huduma za matibabu na kutekeleza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Makonda alisema matumizi ya teknolojia katika usajili wa wagonjwa, utunzaji wa kumbukumbu za kitabibu na ufuatiliaji wa wagonjwa baada ya matibabu ni sehemu ya maono ya Serikali ya kujenga taifa lenye uchumi unaotegemea maarifa, sayansi na teknolojia.

Katika kambi hiyo, Taasisi ya Moyo Mfumo wa teknolojia unaojulikana kitaalamu kama Dozee, una uwezo wa kufuatilia hali ya mgonjwa kwa wakati halisi akiwa amelazwa hospitalini au baada ya kuruhusiwa kurejea nyumbani.

Dozee ni mfumo unaotumia kifaa maalumu kinachowekwa chini ya godoro la mgonjwa na kufuatilia viashiria muhimu vya afya bila kulazimika kuunganisha vifaa vingi moja kwa moja kwenye mwili wake.

Dkt. Kisenge alisema mfumo huo una uwezo wa kufuatilia viashiria muhimu vya afya vya mgonjwa, vinavyojulikana kitaalamu kama vital signs, ikiwemo mapigo ya moyo, kiwango cha oksijeni kwenye damu na shinikizo la damu.

Alisema taarifa zinazokusanywa kupitia mfumo huo zinaweza kumfikia daktari kwa njia ya kidijitali, ikiwemo kupitia simu ya mkononi, hivyo kumwezesha kufuatilia mwenendo wa afya ya mgonjwa hata akiwa nje ya hospitali au anaendelea na shughuli nyingine.

Alifafanua kuwa teknolojia hiyo imelenga kusaidia kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika, hususan vinavyotokea baada ya hali ya mgonjwa kubadilika ghafla akiwa nyumbani baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini.

“Mara nyingi wagonjwa wanaporuhusiwa kwenda nyumbani, hali zao zinaweza kubadilika ghafla. Shinikizo la damu linaweza kushuka, mapigo ya moyo yanaweza kwenda kwa kasi sana au kiwango cha oksijeni kwenye damu kikapungua. Kupitia teknolojia hii, daktari anaweza kupata taarifa kwa wakati na kuchukua hatua mapema kabla hali ya mgonjwa haijawa mbaya,” alisema Dkt. Kisenge.

Alisema mfumo huo hautawanufaisha wagonjwa wa moyo na waliopata huduma za upasuaji pekee, bali unaweza pia kutumika kuwafuatilia wagonjwa wenye matatizo mengine ya kiafya.

Alitolea mfano wagonjwa wenye malaria kali, ambao wanaweza kupata mabadiliko ya ghafla ya mapigo ya moyo, shinikizo la damu na kiwango cha oksijeni kwenye damu.

Kwa mujibu wa Dkt. Kisenge, kufuatiliwa kwa viashiria hivyo kwa wakati kunaweza kuwasaidia wataalamu wa afya kubaini hatari mapema, kumfuata mgonjwa alipo, kumrudisha hospitalini inapohitajika na kumpatia matibabu sahihi.

Alisema uwekezaji katika mfumo huo unaifanya JKCI kuwa miongoni mwa taasisi zinazoongoza katika matumizi ya teknolojia za kisasa za kufuatilia wagonjwa, huku akieleza kuwa teknolojia ya aina hiyo inatumika pia katika nchi zikiwemo India na Marekani.

Dkt. Kisenge alisema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha huduma za afya za kibingwa na ubingwa bobezi nchini.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »