UMOJA WA ULAYA WASAINI MKATABA KUBORESHA UTENDAJI WA BANDARI YA DAR ES SALAAM

December 12, 2024

 Umoja wa Ulaya (EU), kwa kushirikiana na Enabel, UN-Habitat, TradeMark Africa, na Port of Antwerp-Bruges International, wamesaini mkataba wa mradi wa kuboresha utendaji wa Bandari ya Dar es Salaam.


Hafla ya kutia saini ilishuhudiwa na maafisa wa serikali, wakiwemo wawakilishi kutoka Mamlaka ya Bandari Tanzania, Wizara ya Fedha, na Wizara ya Uchukuzi. Mradi huu unaendana na mkakati wa Global Gateway wa EU, ukiwa na malengo ya kuboresha miundombinu muhimu ya usafirishaji, kuongeza ufanisi, uendelevu, na ushindani huku ukichangia malengo mapana ya maendeleo ya Tanzania.

Hafla hiyo ilifanyika wakati wa ziara ya Bw. Hans Stausboll, Mkurugenzi wa Afrika katika Tume ya Ulaya. Ziara yake ilikuwa sehemu ya ujumbe wa ngazi ya juu, ulioshirikisha pia Mazungumzo ya Ushirikiano kati ya EU na Serikali ya Tanzania yaliyofanyika Desemba 10.

Mradi wa Kuboresha Biashara na Usafirishaji Tanzania, ambao utaanza mapema mwaka 2025, una bajeti ya TZS bilioni 41.91 (EUR milioni 15). Utekelezaji wa mradi huo utafanywa na Enabel, UN-Habitat, TradeMark Africa, na Port of Antwerp-Bruges International.

Mradi huu unalenga kuboresha shughuli za bandari kwa kushughulikia changamoto za uendeshaji, kuimarisha usalama na uendelevu wa mazingira. Pia unahamasisha hatua za kuwezesha biashara, kwa mfano kupunguza vikwazo visivyo vya kibiashara na kuboresha taratibu za forodha. Aidha, mradi huu unasaidia mabadiliko ya Tanzania kuelekea mfumo wa usafirishaji wenye kiwango cha chini cha hewa ukaa, hasa kupitia matumizi ya teknolojia ya usafiri wa umeme.

Bw. Stausboll aligusia jinsi mradi huu unavyoakisi na mkakati wa Global Gateway wa EU, akisema:
"Mradi huu ni mfano halisi wa jinsi EU na Tanzania wanavyoshirikiana kuendesha ukuaji endelevu. Kwa kuboresha miundombinu muhimu ya biashara kama Bandari ya Dar es Salaam, tunafungua fursa za kiuchumi za Tanzania na kuimarisha muunganisho wa kikanda."

Aliongeza: "Mkakati wa Global Gateway wa EU unalenga kuboresha miundombinu ambayo ni ya kisasa, safi, na salama. Mradi huu unadhihirisha malengo hayo, na kuhakikisha kuwa Tanzania iko katika nafasi bora ya kukidhi mahitaji ya biashara ya kikanda na kimataifa huku ikikuza maendeleo ya kijani na jumuishi."

Bandari ya Dar es Salaam ni muhimu kwa uchumi wa Tanzania, ikihudumia asilimia 95 ya biashara ya kimataifa ya nchi na kuwa lango kwa majirani wasio na bahari kama Zambia, Rwanda, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Maboresho ya mradi huu yanatarajiwa kuongeza ufanisi wa bandari, kupunguza muda na gharama za kuondoa na kusafirisha bidhaa, na kusaidia mabadiliko ya Tanzania kuelekea mfumo wa usafirishaji wenye kiwango cha chini cha hewa ukaa kwa bidhaa na watu. Mkataba huu unaonyesha ushirikiano thabiti kati ya EU na Tanzania, uliyojengwa juu ya maono ya pamoja ya kuboresha miundombinu ya biashara, kuimarisha muunganisho wa kikanda, na kuendesha ukuaji wa kiuchumi endelevu. 






Share this

Related Posts

Previous
Next Post »