![]() |
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limenyakua tuzo ya utoaji huduma bora za viwango vya kimataifa kupitia utoaji wa huduma zake ndani ya Shirika na nje ya Shirika (The Quality Choice Prize-Vienna 2024). Tuzo hizo hutolewa na Shirika la European Society for Quality Research (ESQR) lenye Makao yake Makuu nchini Switzerland.
Akitoa hotuba ya shukurani mbele ya Menejimenti ya ESQR, wadau mbalimbali wa ubora na viongozi mbalimbali ambao mashirika yao yamenyakua tuzo hizo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) ambaye amemuwakilisha Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) alisema kuwa ushindi wa tuzo hiyo ni kielelezo tosha kuwa Tanzania inaendelea kupiga hatua kubwa katika kutoa huduma bora katika sekta za Utalii na Uhifadhi.
Mhe. Kitandula alisema kuwa, Serikali ya Tanzania itaendela kuhakikisha Hifadhi za Taifa zinatoa huduma bora zinazozingatia uhifadhi wa maliasili kwa kuboresha miundombinu lakini pia kufanya hifadhi hizo kufikiwa kwa muda wote na wageni wa nje na wa ndani ya nchi.
Aidha, Naibu Waziri ameupongeza uongozi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania pamoja na watumishi wote kwa juhudi kubwa wanazofanya katika kuhakikisha kuwa utoaji wa huduma kwa kuzingatia viwango vya ubora wa kimataifa vinakuwa endelevu na kuifanya TANAPA kuendelea kunyakua tuzo hizi za kimataifa.
“Napenda kutumia nafasi hii kuwakaribisha wote mje kwenye nchi yetu ya Tanzania sehemu ambako Hifadhi ya Taifa Serengeti inapatikana, Safu mbalimbali za milima na makundi makubwa na ya kipekee ya wanyama wa asili yanapatina lakini bila kusahau eneo la Ngorongoro lenye mandhari nzuri yenye maajabu pamoja na kisiwa adhimu chenye fukwe nzuri cha Zanzibar”.
TANAPA toka ipate ithibati ya ubora ya kimataifa ya ISO 9001:2015 (Standard on Quality Management System) imekuwa ikinyakua tuzo hizi zinazotolewa na “European Society for Quality Research (ESQR)” kwa mara ya tano sasa mfululizo tangu mwaka 2020.
Tuzo za ESQR hutolewa kwa kuzingatia kura ambazo hupigwa na wateja mbalimbali, maoni ya wateja, tafiti za utoaji huduma kwa kuzingatia viwango vya ubora vya kimataifa na utafiti wa masoko ya utalii.
EmoticonEmoticon