DAR ES SALAAM*
*14 DISEMBA, 2024*
*RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameishauri Bodi mpya ya Wadhamini ya Taasisi ya Benjamin William Mkapa kuhakikisha inaendelea kuwa chombo cha kuaminika na Watanzania kwenye kuimarisha sekta ya afya ndani na nje ya nchi kama ilivyo Dira ya Taasisi hiyo.*
Rais Dk Mwinyi ametoa tamko hilo alipozindua Bodi Mpya ya BMF hafla iliofanyika Ukumbi wa BMF Kawe, jijini Dar es Salaam.
Rais Dk. Mwinyi ambae ni Msarifu wa taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation ameeleza kuwa ni vema kwa sifa za wajumbe wa taasisi hiyo kuendelea kudumu ndani ya taasisi ili kuwavutia washirika zaidi na kuhakikisha ukuaji endelevu wa kuwahudumia walengwa wa taasisi hiyo.
Rais Dk. Mwinyi amefafanua kuwa Mpango Mkakati wa Taasisi hiyo utakaodumu kuanzia Julai 2024 hadi Juni 2030 utategemea Bodi na Menejimenti katika kutekeleza na kufikia malengo yaliowekwa na kusisitiza umuhimu wa kudumisha rekodi nzuri ya utawala Bora, Uongozi mahiri, Utendaji wa kazi wa taasisi hiyo.
Rais Dk. Mwinyi ameeleza kufarijika kwake kwa BMF kuwa na sifa ya kupata hati safi ya ukaguzi wa hesabu kwa miaka 17 mfululizo kupitia wakaguzi wa ndani na wale wa kimataifa na kusisitiza sifa hiyo kuendelezwa ili kujenga imani kwa wadau wa ndani na nje ya nchi.
Aidha, ameipongeza taasisi ya Benjamin William Mkapa kwa kuendelea kuwekeza kwa mafanikio kwenye Kampuni tanzu ya "Imara Horizon Company" na kuipongeza Bodi na Menejimenti kwa kuwekeza kwa hali na Mali.
Rais Dk.
Mwinyi ambae pia ni Msarifu wa BMF amempongeza Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa "Imara Horizon Company", Balozi John Ulanga na wajumbe wenzake kwa kufanikisha Ujenzi wa Jengo la "Mkapa Health Plaza" kwa kipindi cha miezi 12 tangu alipoweka jiwe la Msingi Julai 2023.
Rais Dk. Mwinyi amewashukuru Wajumbe wa bodi iliomaliza muda wake kwa mafanikio makubwa ya BMF na kutekeleza majukumu yao kwa matokeo makubwa na Kuisisitiza bodi mpya aliozindua chini ya Mwenyekiti wake mpya Balozi Liberata Mulamula kufanya kazi kwa Ushirikiano, umahiri, weledi na Uzoefu kuendelea kuifanya Taasisi ya Benjamin William Mkapa Foundation kuwa taasisi bora na tegemeo kwa Watanzania wakati wote.
Akizungumza katika Hafla hiyo, Mwenyekiti Mpya wa BFM Balozi, Liberata Mulamula ameahidi kwa bodi hiyo kufanya kazi kwa karibu na Serikali zote mbili za SMT na SMZ katika kufikia malengo na Dira ya taasisi Hiyo
Rais Dk. Mwinyi alikabidhi vyeti maalum vya Ushirikiano na Shukrani kwa Wajumbe wa bodi ya BMF waliomaliza muda wao pamoja kukabidhi nyaraka muhimu kwa Bodi Mpya kwa ajili ya utekelezaji ikiwemo Ripoti maalum ya Miaka mitano .
Hafla hiyo ya uzinduzi wa Bodi mpya ya BMF ipia ilihudhuriwa na Mjane wa Hayati Benjamin Mkapa, Mama Anna Mkapa.
EmoticonEmoticon