Na Kassim Nyaki, Ngorongoro Crater.
Tarehe 15 Desemba 2024 Kreta ya Ngorongoro imepambwa na tukio adhimu na la kihistoria la maharusi wa Kitanzania kufunga ndoa ndani ya Hifadhi huku wakipunga upepo mwanana kwenye mazingira asilia yaliyozungukwa na wanyama mbalimbali wakiwemo Big 5.
Bw. Kelvin Mwakaleke na mkewe
Jackline Nyalu wamefunga Ndoa ndani ya Kreta ya Ngorongoro wakisindikizwa na wazazi, ndugu, jamaa na marafiki huku wakishuhudiwa na macho ya Wanyama mbalimbali wakiwemo Simba, Faru, Tembo, Nyati, Chui, Pundamilia, Nyumbu, Thomson Gazelle, ambao wamekuwa mashuhuda wa tukio hilo lililofanyika pembeni mwa bwawa maarufu la Ngoitoktok wakati huo Viboko wakinogesha shughuli hiyo kwa kuogelea.
Akielezea tukio hilo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Mariam Kobelo anayesimamia huduma za Utalii na Masoko NCAA ameeleza kuwa; "Leo ni siku ya furaha na ya kipekee isiyosahaulika, tumeshuhudia tukio adhimu na akramu lenye baraka za Mungu kwa maharusi hawa kufunga ndoa kwenye bustani ya Eden (Ngorongoro Crater).
"Hili ni jambo jipya na la kwanza katika historia ya NCA na limechagizwa na juhudi za Utangazaji wa vivutio vya utalii vinavyopatikana ndani ya NCA ambavyo vimeendelea kuibua chachu kwa watanzania wengi, ndio maana unaona leo tumeona zao jipya la utalii. Tunaendelea kuwakaribisha wananchi wengine kuja hifadhi ya Ngorongoro kwa matukio kama haya" alifafanua Kamishna Kobelo.
Kufunga ndoa ndani ya hifadhi ni fursa muhimu katika kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Ngorongoro hali inayoamsha ari kwa watalii wa ndani kuongezeka na kuchangia mapato ya Serikali.
Akielezea tukio hilo akiwa na nuru ya tabasamu na furaha Bwana harusi Kelvin Mwakaleke akiwa na mkewe Jackline ameeleza kuwa kufunga ndoa ndani ya hifadhi ilikiwa ndoto yake ambayo hatimae imetimia.
"Nilimuomba Mungu kuniongoza kufanikisha tukio hili, kufunga ndoa kreta ni uzoefu ambao siwezi kuusahau, ni eneo lenye vivutio vya kila aina kwa mtu yoyote kutembelea, lina uzuri wa asili wanyama wengi na uoto wa asili uliohifadhiwa vema, mimi, mke wangu na ndugu wachache tuliounganika hapa tutakuwa mabalozi wa kuitangaza hifadhi ya Ngorongoro" alisema Bw. Mwakaleke.
Aidha, alishukuru kwa huduma nzuri iliyotolewa na wahifadhi wote waliokuwa bega kwa bega kuhakikisha wanakuwa salama na kufurahia mandhari na kukamilisha ndoa yao.
#WedinWild
#merryandwild
#Ngorongoroawaits
#visitngorongoro
#unforgettableexperiences
EmoticonEmoticon