Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda akikata keki alıposhiriki Maadhimisho ya miaka thelathini ya Umoja wa Watanzania wanaoishi nchini Botswana (ATB) yaliyofanyika jijini Gaborone tarehe 2 Novemba, 2024
Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Pinda ameshiriki Maadhimisho ya miaka Thelathini ya kuanzishwa
kwa Umoja wa Watanzania wanaoishi nchini Botswana (ATB) yaliyoandaliwa na
Ubalozi wa Tanzania nchini Botswana na Jumuiya hiyo yaliyofanyika jijini Gaborone tarehe 2 Novemba, 2024.
Akizungumza katika
hafla hiyo Mhe. Pinda amesema Serikali ya Tanzania inabuni mbinu na
mikakati mahsusi kwa lengo la kuwawezesha Diaspora kuendelea kuchangia zaidi
katika maendeleo ya taifa kupitia maeneo ya kimkakati na kuwasihi wachangamkie fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji
zinazopatikana nyumbani.
Mhe. Pinda pia amewasihi Diaspora hao kutumia mifumo rasmi ya kutuma
fedha nyumbani (remittances) ili kuiwezesha
Serikali kuwa na taarifa na takwimu sahihi za mchango wa disapora kwa Taifa lao.
“Nichukue nafasi hii kuwajulisha kuwa Serikali iko katika hatua ya maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya
Mwaka 2050, niwasihi Diaspora mtumie ujuzi na uzoefu mlioupata huku ugenini kwa
kutoa maoni yenu kwa ajili ya Dira ya mpya ya Maendeleo ya Mwaka 2050 kwani kwa
kufanya hivyo mtaliwezesha Taifa kupata dira itakayolifikisha kule kunakotarajiwa, alisisitiza Mhe. Pinda.
Pia amewasihi Diaspora hao
kuendelea kujisajili katika mfumo wa kidijitali ujulikanao kama Diaspora Digital Hub (DDH) ili kuiwezesha
Serikali kuwa na takwimu sahihi za Diaspora wake na kufanikisha
maamuzi ya kisera kwa kuzingatia idadi na mchango wa dispora kwa Taifa.
Mhe. Pinda amewaomba Disapora hao wa Botswana kuendelea
kuitetea nchi yao, kudumudisha mila, desturi na tamaduni zao, kupendana,
kusadiana, kuinuana na kutatua changamoto kwa pamoja huku wakiendelea
kushirikiana na Balozi wao aliyepo Pretoria, Afrika Kusini kama mlezi wao na kufuata
sheria za nchi mwenyeji na wakumbuke kuwa nyumbani kwao ni Tanzania.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa
pia na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Balozi Said Shaib Mussa, Balozi wa Tanzania Afrika Kusini
anayewakilisha pia nchi za Botswana na Lesotho Mhe. James Bwana; Balozi Dkt. Salim Omar Othman;
Mwambata wa Biashara na Uwekezaji katika Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika
Kusini Bi. Happyness Godfrey pamoja na Watanzania wanaoishi nchini
Botswana.
Maadhimisho hayo yalitanguliwa na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa ATB ambao uliambatana na Uchaguzi wa Viongozi wa ATB kwa Muhula mpya ambapo Bw. Naiman Kissasi alichaguliwa kuwa Mwenyekiti , Peace Byengozi alichaguliwa kuwa Katibu pamoja na Viongozi wengine wa Kamati Tendaji. Kupitia Maadhimisho hayo Benki ya CRDB pamoja na Kampuni ya KC LAND walipata fursa ya kunadi huduma zao mahususi kwa ajili ya Diaspora wa nchini Botswana.
Mhe. Pinda yuko nchini
Botswana kwa ajili ya kuongoza misheni ya Uangalizi ya Uchaguzi. Mkuu wa
Botswana ya SADC (SEOM) uliofanyika nchini humo tarehe 30 Oktoba, 2024 ambako Chama
cha Upinzani cha UDC kilipata ushindi wa zaidi ya viti 31 vya Bunge la nchi
hiyo na hivyo kukiondoa madarakani chama tawala cha BDP kilichokuwa kikiongozwa
na aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Mhe. Mokgweetsi Masisi
EmoticonEmoticon