KFW YAIFADHILI TAWA MAGARI YENYE THAMANI YA ZAIDI YA TZS MILIONI 600

November 14, 2024



📍 *Yatarajia kuongeza misaada zaidi kuimarisha shughuli za Uhifadhi*


Na Beatus Maganja, Morogoro.


Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW) kupitia Mradi wa Afue ya UVIKO 19 "Emergency and Recovery Support for Biodiversity Tanzania (ERB)" ulio chini ya Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS),leo tarehe 14 Novemba, 2024, imekabidhi msaada wa magari mawili (2) aina ya ISUZU FVZ yenye thamani ya zaidi ya TZS Millioni 600 kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa ajili ya kusaidia shughuli za uhifadhi katika Pori la Akiba Selous.


Akizungumza mara baada ya kupokea magari  hayo katika hafla iliyofanyika Ofisi za Makao Makuu ya TAWA Mkoani Morogoro Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mabula Misungwi Nyanda amezishukuru KFW na FZS kwa kazi nzuri wanazozifanya katika kuimarisha uhifadhi nchini hususani Kwa msaada walioutoa na kusisitiza kuwa magari hayo ni nyenzo muhimu sana katika kuboresha utendaji wa TAWA.



"Tunawashukuru wenzetu wa KFW na FZS pamoja na washirika wengine wa uhifadhi kwa kuendelea kutuunga mkono katika kuhakikisha tunaimarisha uhifadhi katika maeneo tunayoyasimamia" amesema Kamishna Mabula.


"Magari haya yatatumika Kwa kazi nyingi ikiwemo ujenzi wa miundombinu Kwa ajili ya uhifadhi na utalii " ameongeza Kamishna Mabula.


Aidha Kamishna Mabula amewasisitiza Wakuu wa Kanda husika kuhakikisha  magari hayo yanatumika vizuri na kufanyiwa ukarabati kwa wakati ili yaendelee kudumu.



Naye, Meneja Mradi wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani kwa Bara la Afrika, Bw. Christian Weidner amesema KFW inajisikia fahari kutoa mchango wao wa uhifadhi katika mojawapo ya hifadhi kubwa Afrika na kuomba magari hayo yapelekwe  Hifadhi ya Selous ili kuweza kuungana na timu  inayoshughulika na miundombinu.


Aidha amesema Mradi wa Afue ya UVIKO 19 wenye thamani ya EURO Millioni 35 ambao unatekelezwa kwa ubia Kati ya Shirika la Frankfurt Zoological Society, TAWA na TANAPA uliletwa nchini Kwa lengo la kusaidia katika shughuli za uhifadhi baada ya janga la UVIKO 19.



Amesema kutokana na changamoto ya janga hilo Serikali ya Tanzania ikishirikiana na Serikali ya Ujerumani walikubaliana kusaidia shughuli za uhifadhi kwenye Pori la Akiba Selous.



Christian Weidner amesisitiza kuwa Mradi huo utaendelea kutoa misaada mbalimbali Kwa ajili ya kusaidia shughuli za uhifadhi katika Pori la Akiba Selous.



"Ziko rasilimali zingine ambazo zitatolewa na mradi huu ikiwemo matrekta, boti za doria pamoja na manunuzi ya vifaa mbalimbali Kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa shughuli za TAWA kupitia Pori la Akiba Selous" amesema Christian

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »